HOTUBA YA MHESHIMIWA PAUL MAKONDA MKUU WA MKOA WA DAR ES SALAAM ILIYOSOMWA NA MKUU WA WILAYA YA ILALA MHESHIMIWA SOPHIA MJEMA KWENYE UFUNGUZI WA MKUTANO WA WADAU WA MASUALA YA HUDUMA YA MAJI KATIKA MKOA WA DAR ES SALAAM NEW AFRICA HOTEL 30 AUGUST 2017.
Katibu Tawala (M) na Watumishi kutoka Sekretariate ya Mkoa wa DSM,
Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Dsm,
Wakurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Temeke , Ubungo, Kigamboni na Kinondoni,
Mkurugenzi Mkuu DAWASA na DAWASCO,
Wadau wa Maji na Wadau wa Maenedeleo Mkoa wa DSM,
Watumishi wa DAWASA na DAWASCO,
Ndugu Wananchi, Waandishi wa Habari,
Mabibi na Mabwana,
Ninafuraha kubwa kuwa hapa leo hii kushiriki nanyi katika kikao hiki muhimu cha Wadau wa Maji na Usafi wa Mazingira katika Mkoa wetu wa Dar es Salaam. Kama alivyoeleza Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es salaam, kikao hiki nilitaka kifanyike mara tu baada ya kumaliza Maadhimisho ya kilele cha Wiki ya Maji Mwezi Machi mwaka huu 2017 ambapo niliwaagiza watendaji wa Sekta ya Maji wafanye maandalizi ya kikao hiki. Lakini watendaji walioko chini ya Ofisi yangu walinishauri nifanye kwanza ziara ili kuona maendeleo ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya majisafi na majitaka katika Mkoa wetu. Nami nilikubaliana nao na nikafanya ziara hizo kama ambavyo Katibu Tawala amefafanua.
Ndugu Washiriki wa Kikao, katika ziara nilizofanya nilitembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali kupitia Mamlaka ya maji, DAWASA. Katika ziara hiyo niliweza kujifunza mambo mengi sana kuhusu mipango mbalimbali ya Serikali inayoendelea hivi sasa ya kuwapatia Wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam huduma ya maji. Niliona jitihada kubwa zinazofanywa na Mamlaka ya Maji ya DAWASA za kusimamia miradi hiyo kwa lengo la kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma ya Majisafi katika Jiji letu. Pamoja na jitihada zinazofanywa na Serikali yetu kupitia Mamlaka ya DAWASA nimegundua bado kuna mapungufu mengi na malalamiko mengi kuhusu huduma ya maji kwa wananchi wetu.
Hivi sasa maji yanayozalishwa ni mengi sana ambayo yanaweza kukidhi zaidi ya asilimia 90 ya Wananchi wote lakini ukweli ni kwamba maji hayo bado hayajafika kwa Wananchi kutokana na uhaba wa mtandao wa mabomba hususan ni maeneo yaliyoendelezwa miaka ya hivi karibuni na yale yaliyoko pembezoni mwa Jiji.
Ndugu Washiriki wa Kikao, Kufuatia changamoto nilizoziona katika ziara yangu na kupitia mikutano niliyofanya maenneo mbalimbali ya Jiji ndio maana nikaamua niwaite Wadau mbalimbali ili tujadili kwa pamoja namna ya kuzikabili changamoto hizi ili tuweze kuendana na malengo ya Serikali ya kuhakikisha kuwa asilimia 95 ya wananchi wanapata huduma ya maji ifikapo mwaka 2020.
Lakini kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ambapo maji yanayozalishwa hivi sasa ni mengi sana kukidhi zaidi ya asilimia 90 ya mahitaji; ndio maana mimi na wataalamu wangu tukasema kuwa wananchi wa Mkoa wa Dar es salaam wanaweza kupata huduma ya Majisafi na salama wote (100%) ifikapo 2020 “HUDUMA YA MAJI MKOA WA DAR ES SALAAM KWA WOTE IFAKAPO 2020” iwapo tutakaa na Wadau wote kuona namna bora na ya ufanisi wa kuyasambaza maji yote yanayozalishwa hivi sasa.
Leo tumekutana na baadhi tu ya Wadau wetu wa Maendeleo ambao wamekuwa wanatusaidia sana katika suala zima la kuhakikisha tatizo la maji linapungua.
Ndugu Washiriki wa Kikao, Napenda kutoa shukrani za pekee kwa wadau wetu WaterAid kwa kufadhili kikao hiki. Aidha, napenda pia kuwashukru wadau mbalimbali bila kuwasahau Benki ya Dunia na Korea ya Kusini ambao wamekubali kufadhili miradi mikubwa ya maji na usafi wa mazingira Katika Jiji la Dar es Salaam. Aidha, natambua kuwa Wadau wote walioshiriki hapa na ambao wameshindwa kushiriki siku ya leo najua wanatambua kuwa wananchi wa Dar es Salaam wana kiu ya huduma na wote kwa pamoja tunapaswa kuhakikisha kuwa wanapata huduma bora ya maji. Kwa juhudi zenu za kusaidia katika upatikanaji wa huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira kwa Mkoa wetu. Kwa pamoja nawaomba tuzidi kushirikiana katika kutatua changamoto za upatikanaji wa huduma ya maji na usafi wa mazingira ili kuhakikisha kuwa malengo tuliojiwekea yanafikiwa kwa wakati.
Ndugu Washiriki, Ni matumaini yangu kuwa kwa siku hii ya leo tutapata fursa ya kuelewa na kushiriki katika mijadala ya namna ya kukabiliana na changamoto za utoaji wa huduma ya Maji. Nina imani kubwa sana kuwa Mkutano huu utatoa maazimio ambayo yatakuwa suluhu ya matatizo ya maji katika Jiji letu.
Baada ya kusema hayo natamka rasmi kuwa Mkutano wetu umefunguliwa rasmi.
Asanteni kwa kunisikiliza naomba sasa tuendelee na RATIBA.
MAJI NI UHAI NA USAFI WA MAZINGIRA NI UTU
“HUDUMA YA MAJI MKOA WA DAR ES SALAAM KWA WOTE IFIKAPO 2020”
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa