Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe.Paul Makonda leo amepokea Pikipiki za kisasa 10 kwa ajili ya Askari wa Usalama Barabarani zenye thamani ya Shilingi Million 400 kutoka kampuni ya utengenezaji wa Pikipiki ya TONGBA ya China.
Hatua hiyo inakuja baada ya RC Makonda kutafuta kampuni hiyo na kuwasilisha ombi la kupatiwa Pikipiki za kisasa kwa ajili ya kuongoza Misafara ya Viongozi, Misiba na kuwahisha Wagonjwa waliozidiwa Hospitalini ambapo kampuni hiyo ilipokea kwa mikono miwili ombi hilo kwa kutoa Pikipiki hizo.
Mhe. Makonda amesema lengo lake ni kuboresha Mazingira ya utendaji kazi wa Jeshi la Polisi kwa kuhakikisha Askari wanakuwa na vifaa vya kutosha ambapo hadi sasa amefanikiwa kupata Baiskeli 500, Pikipiki za kawaida 200, Kompyuta 100, Pikipiki za Trafic 10 na kufanya maboresho ya Magari ya Jeshi hilo yaliyokuwa yameharibika.
Aidha Mhe. Makonda amemuagiza aliyekuwa Kaimu Kamanda wa Polisi kanda maalumu ya Dar es salaam kuwakamata Askari wote waliobainika kushirikiana na wauzaji wa Dawa za kulevya na wale wanaobambikizia Wananchi kesi kukamatwa ndani ya masaa matano.
Agizo hilo limekuja baada ya hivi karibuni Msamaria mwema kutoa taarifa za uwepo wa muhusika wa Dawa za kulevya kwenye moja ya Hotel na Askari walipofika kwenye Hotel hiyo wakamkamata na kupewa Rushwa baada ya muda Mtuhumiwa akaachiliwa na kurudi kwenye Hotel kisha kufanya fujo kumtafuta aliyetoa taarifa na baada ya Makonda kufika na kuangalia Camera za CCTV wakawabaini Askari hao.
Pamoja na hayo amesema wapo Askari waliomkamata Mwananchi akiwa na Mpenzi wake kwenye Gari kisha kuwapiga Picha za Utupu na kuwalazimisha watoe kiasi cha Million Tano iliwasisambaze Picha hizo kitendo ambacho ni kinyume na Sheria ambapo Mheshimiwa Makonda amesema hawezi kuruhusu vitendo kama hivyo vitendeke kwenye Mkoa wake na kuongeza kuwa anataka kuona Sheria na Haki vinatendeka kwa Wananchi.
Mhe. Makonda pia amebaini uwepo wa Askari wa Uwanja wa Ndege wanaoshirikiana na Raia wa China kusafirisha Kobe na Wanyamapori na Askari wanaowabambikia kesi wananchi ikiwemo wale wanaowakamata watu kwenye sehemu za mapumziko.
Amesema hatokubali kuona Askari wachache wanaotumia Magwanda kuwanyanyasa Wananchi na kuchafua taswira ya Jeshi la Polisi na kufanya Wananchi kushindwa kutoa ushirikiano.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa