Mashirika ya Umma na Sekta binafsi kote nchini yametakiwa kuhakikisha yanashirikiana bega kwa bega na Serikali katika kumuwezesha mwanamke kujikwamua kiuchumi na kimaendeleo.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mama Janet Magufuli, Mke wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania alipokuwa Mgeni rasmi siku ya maadhimisho ya mwanamke duniani yenye kauli mbiu isemayo "Kuelekea Uchumi wa viwanda tuimarishe usawa wa Jinsia na uwezeshaji wa wanawake vijijini."
Amesema kufuatia kauli mbiu hiyo wanawake wanatakiwa kujengewa uwezo ikiwemo elimu ya ujasiriamali, mafunzo, ili kupata mbinu za kuwekeza, mitaji pamoja na maeneo kwa lengo la kumsaidia mwanamke kujikwamua kiuchumi.
Ameongeza kuwa lengo la siku ya wanawake duniani ni kutukumbusha harakati na mafanikio yaliyokwisha fanyika katika kumkwamua mwanamke dhidi ya unyanyasaji, hali duni, kutelekezwa na kuhakikisha haki yake inapatikana, inaheshimiwa na kuenziwa.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar Es salaam Mh Paul Makonda alipotoa nasaha zake wakati wa maadhimisho hayo amesema wanawake wa Mkoa wa Dar Es Salaam wanajitahidi Sana katika kuhakikisha wanaendana na kasi iliyopo ya uchumi wa viwanda.
Amebainisha kuwa katika Mkoa wake kunajumla ya vicoba 2748 vyenye mtaji wa takribani bilioni 10.78 ambavyo vinaendeshwa na wanawake.
Aidha amebainisha kuwa katika mkoa wake unajumla ya idadi ya watu milioni 6, na kati ya hao wanawake ni wengi kuliko wanaume, hivyo ni jeshi kubwa ambalo likiwezeshwa linaweza.
Maadhimisho haya ya siku ya wanawake yaliyofanyika kimkoa katika Manispaa ya Ubungo katika ukumbi wa Mlimani city yalihudhuriwa na viongozi wa Vyama na Serikali,pamoja na vikundi mbalimbali vya wajasiriamali kutoka Manispaa ya Kinondoni, Ilala, Temeke, Kigamboni na Ubungo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa