Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Paul C. Makonda amekabidhi Mwenge wa Uhuru kwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Mhandisi Evarist Ndikilo mapema leo asubuhi baada ya kukaa ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam kwa muda wa siku tano kuanzia tarehe 27/05/2017 mpaka tarehe 31/05/2017
Makabidhiano hayo yamefanyika katika Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere Terminal One na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali wakiwemo Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Dar es Salaam, Viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Wahe. Madiwani, Wakurugenzi wa Halmashauri za Jiji la Dar es Salaam, Makatibu Tawala wa Wilaya zote, Wadau mbalimbali wa Maendeleo, Watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa na Vikundi vya Hamasa vya Mkoa wa Dar es Salaam.
Awali, Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alianza kwa kumshukuru Mungu na kuwakaribisha wote waliofika kwa ajili ya tukio muhimu la makabidhiano ya Mwenge wa Uhuru.
Katika hotuba yake Mhe. Paul Makonda alieleza jinsi Mwenge wa Uhuru ulivyotimiza azma yake kwa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kukagua miradi yenye thamani ya Tshs 244,392,530,334/= ambapo miradi mikubwa 12 ilizinduliwa, miradi 5 iliwekewa mawe ya msingi, na miradi 11 ilitembelewa na kufunguliwa.
Mhe. Paul Makonda alieleza kuwa aliupokea Mwenge wa Uhuru ukitokea katika Mkoa wa Lindi na umefanya mambo mengi makubwa na mazuri kwa Wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam, hivyo ameukabidhi Mwenge huo kwa Mkoa wa Pwani kwa moyo mweupe ili ukazindue, kutembelea na kuweka Mawe ya Msingi katika Miradi mbalimbali Mkoani humo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Mhandisi Evarist Ndikilo amesema kuwa ameupokea Mwenge wa Uhuru na ameahidi kuukimbiza katika Wilaya zote saba zilizopo katika Mkoa huo sambamba na kuzindua, kutembelea na kuweka Mawe ya Msingi katika Miradi itakayogharimu zaidi ya Shilingi Bilioni themanini na tano.
Mbio za Mwenge wa Uhuru katika Mkoa wa Dar es Salaam zimekua kichocheo kikubwa katika kuhamasisha Maendeleo, Uzalendo, Umoja, Mshikamano na Kudumisha Amani.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa