HOTUBA YA MGENI RASMI KWENYE MAADHIMISHO YA WIKI YA ELIMU MKOA WA DAR ES SALAAM TAREHE 14/12/2017
Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya;
Waheshimiwa Wastahiki Mameya wa Manispaa;
Ndugu Waandaaji wa Maadhimisho haya
Waheshimiwa Wenyeviti wa Kamati za Huduma za Uchumi, Afya na Elimu wa Halmashauri za Manispaa;
Ndugu Makatibu Tawala wa Wilaya;
Ndugu Wakurugenzi wa Manispaa;
Ndugu Wawakilishi wa Wakuu wa Shule za Serikali na zisizo za Serikali;
Ndugu Wawakilishi wa Asasi mbalimbali;
Waandishi wa Habari;
Mabibi na Mabwana;
Ndugu Wadau na Wageni waalikwa;
Ninayo furaha kuwa pamoja nanyi katika Maadhimisho ya Wiki ya Elimu katika Mkoa wetu na sote tukiwa na afya njema; ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu.
Niwapongeze wote mliofika mahali hapa kwa kazi mbali mbali ambazo mmekuwa mkizifanya zinazouletea heshima Mkoa wetu na Taifa kwa ujumla.
Ninatambua mchango wa kila mmoja katika kuimarisha na kuinua kiwango cha taaluma na ufaulu katika Mkoa wa Dar es Salaam, leo hii tumekusanyika tukifurahia matokeo mazuri ya juhudi zetu. Hongereni sana.
Ndugu Wadau na Wageni waalikwa;
Ninaishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuwa na dhamira ya dhati ya kuhakikisha kila mtoto mwenye umri wa kwenda shule anaandikishwa kupitia Mpango wa Elimu msingi bila Malipo, Waraka wa Elimu Namba 2 wa mwaka 2016 umezingatiwa ambapo tunashuhudia jinsi ongezeko la usajili wa wnafunzi kwenye shule za umma/Serikali.
Aidha, Serikali imekuwa ikishirikisha Wadau wa Elimu kwa kutoa fursa ya kuwekeza katika Sekta ya Elimu tunathamini kila jitihada zinzotekelezwa na Taasisi zisizo za Serikali ambazo zinaisaidia Serikali katika kufikia malengo mbalimbali hata leo tunaona kwa vitendo utekelezaji wa jambo hili. Ninatoa rai kwa Wadau wote tuendelee kuiunga mkono Serikali yetu.
Ndugu Wadau na Wageni waalikwa;
Nimefahamishwa kwamba lengo la maadhimisho haya ni kutoa tuzo kwa waliofanya vizuri katika usimamizi wa utekelezaji wa Mtaala wa Elimu na waliofanya vizuri katika matokeo ya mtihani ngazi ya Upimaji wa Darasa la Nne na Kidato cha Pili, katika Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi na Kidato cha Nne mwaka 2016.
Ndugu Wadau na Wageni waalikwa;
Serikali imefanikiwa kuondoa changamoto ya uhaba wa miundombinu katika Shule za Msingi za Mkoa wetu, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John P. Magufuli ametoa fedha Sh.2,106,770,000/= ambazo zimetumika kujenga vyumba vya madarasa 121, matundu ya vyoo 14, Ofisi za Walimu na samani za Ofisi tano (5).
Aidha, Serikali imekuwa ikitoa fedha za ujenzi na ukarabati wa Shule za Sekondari na Msingi kupitia Programu ya Elimu ya Lipa Kulingana na Matokeo kwa kifupi (EP4R) ambao matokeo yake ni mazuri ni mpango endelevu. Niwapongeze Wakuu wa Shule kwa kusimamia vizuri matumizi ya fedha hiyo.
Katika kuboresha mazingira ya makazi ya walimu, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa kushirikiana na Kampuni ya Property International wameandaa mpango wa upatikanaji wa viwanja vya makazi kwa ajili ya walimu. Jumla ya walimu 872 wa Shule za msingi na Sekondari wameonesha nia ya kupata viwanja hivyo.
Aidha, Mkuu wa Mkoa ameanzisha kampeni ya kuboresha mazingira ya mazuri ya kazi ya ufundishaji na ujifunzaji kwa kutoa kipaumbele kwa ujenzi wa majengo ya utawala 402. Kwa shule za msingi 295 na Sekondari 107 ambapo katika awamu hii ya kwanza ujenzi wa majengo 100 yaani 73 ni kwa shule za msingi na 27 sekondari unaendelea.
Mkoa umefanikiwa kusimamia utaratibu wa usafiri kwa Walimu kwenda na kurudi kazini bila malipo ya nauli.
Aidha, jitihada za Mkuu wa Mkoa katika kuhakikisha kuwa walimu wa sayansi wanatosheleza katika shule zetu za serikali. Jumla ya maombi 352 yalipelekwa Ofisi ya Rais – TAMISEMI na hadi sasa walimu 75 wamepata leseni ya muda kwa miaka miwili, hivyo Wakurugenzi wa Halmashauri waandae utaratibu wa kuona namna watakavyopata vyanzo vya malipo kwa ajili ya walimu hawa.
Ndugu Wadau na Wageni waalikwa;
Baada ya maelezo haya, nirudie tena kuwapongeza wote kwa dhamira njema ya kuendelea kulitumikia na kulijenga Taifa letu la Tanzania.
Sasa ninatamka kuwa nipo tayari kutoa tuzo kama zilivyoandaliwa kwa makundi mbalimbali.
Asanteni kwa kunisikiliza.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa