- Kwa Mkoa wa Dar es Salaam Kingatiba itatolewa katika Halmashauri tatu (3)
- Rai yatolewa kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kupata Kingatiba ya Matende na Mabusha
- Kingatiba hiyo inatolewa kwa watu wote, watoto kuanzia miaka 5 na kuendelea
Katibu wa Afya Mkoa wa Dar es Salaam Sister Methew kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt Rashid Mfaume leo Octoba 8, 2021 amefungua warsha ya Wanahabari kuhusu ugawaji wa kingatiba za kudhibiti ugonjwa wa Matende na Mabusha kwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Kinondoni na Temeke
Warsha hiyo imefanyika katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa Ilala boma, Dar es Salaam.
Akifungua warsha hiyo Katibu wa Afya Mkoa Sister Methew amesema Kingatiba dhidi ya Matende na Mabusha kwa Mkoa wa Dar es Salaam itafanyika katika Halmashauri 3, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Kinondoni na Temeke kuanzia Octoba 24 - 29 , 2021
Sister Methew amesema Kingatiba hiyo itafanyika katika maeneo mbalimbali yenye mikusanyiko ikiwemo mashuleni na kwenye vyuo.
Kwa kutambua umuhimu wa Wanahabari Sister Methew amesema ni daraja muhimu katika utoaji elimu kwa Umma na taarifa sahihi juu ya Kinga tiba dhidi ya Matende na Mabusha au Ngirimaji na ndio maana Wanahabari wamekuwa kundi mojawapo kupatiwa mafunzo ili wawe na uelewa na wakaelimishe Jamii.
Aidha Sister Methew ametoa Rai kwa Jamii hususani katika Halmashauri hizo 3 kujitokeza kupata kingatiba hiyo ambayo ni bure na tayari Mkoa umeshajipanga vizuri kutoka huduma kwa wananchi.
Kwa upande wa watoa mafunzo Bwana Oscar Kaitaba Afisa Mpango wa Taifa wa kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele, kwa niaba ya wataalam wengine amesema Jamii inapaswa kuelimishwa juu ya athari za Matende na Mabusha na Wanahabari ndio Wadau muhimu kupitia warsha hiyo wamepata uelewa juu ya Chanzo, Maambukizi, Ueneaji, na Kingatiba
Hivyo Jukumu la Wanahabari ni kwenda kuelimisha Jamii ili hatimaye kutokomeza kabisa Magonjwa hayo kwa kuwa watu watakuwa wameshajipatia Kingatiba hiyo.
Ifahamike kuwa kwa muda mrefu jamii imekuwa ikiteseka na magonjwa hayo pasipo kujua Kingatiba yake ipo na wengine wamekuwa wakiweka siri sasa ni wakati muafaka kwa Jamii kutumia fursa hii adhimu ya Kingatiba dhidi ya Matende na Mabusha au Ngirimaji
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa