HOTUBA YA MKUU WA MKOA WA DAR ES SALAAM MHE. PAUL C. MAKONDA KATIKA KILELE CHA MADHIMISHO YA SIKU YA MAZINGIRA DUNIANI NGAZI YA MKOA
VIWANJA VYA MNAZI MMOJA, TAREHE 05/06/2017
Katibu Tawala wa Mkoa,
Wah. Wakuu wa Wilaya za Ilala, Kinondoni na Temeke,
Wah. Mameya
Wah. Madiwani
Wakurugenzi wa Halmashauri,
Watendaji wa Serikali,
Wadau wote wa Mazingira
Wageni waalikwa,
Mabibi na Mabwana.
Ndugu Wananchi,
Leo hii tunaungana na Wenzetu Duniani kote kuadhimisha siku ya Mazingira Duniani. Siku hii huadhimishwa kila mwaka tarehe 05 ya mwezi Juni, Duniani kote. Lengo kuu la Maadhimisho ya siku ya Mazingira mwaka huu ni kufanya tathmini ya Mazingira, kubaini changamoto zinazoikabili Sekta ya Mazingira na kutoa mwelekeo wa kupambambana na changamoto hizo ili kuwa na Mazingira bora na endelevu.
Ndugu Wananchi,
Mwaka huu Maadhimisho ya Kitaifa hapa nchini yanafanyika Mkoani Mara katika kijiji cha Butiama ili kumuenzi hayati Mwalimu Julius Nyerere katika dhana ya kuhifadhi mazingira. Kauli mbiu ya Mwaka huu Kitaifa ni ″Hifadhi ya Mazingira; Mhimili kwa Tanzania ya Viwanda‶. Kimataifa ni ″Mahusiano endelevu kati ya Binadamu na Mazingira‶. (″Connecting People to Nature‶.)
Ndugu Wananchi,
Maadhimisho haya hutanguliwa na shughuli mbalimbali zinazohamasisha utunzaji mazingira ambazo hufanyika katika maeneo mbalimbali kuelekea siku ya kilele. Kwa wiki hii ya maadhimisho, Halmashauri za Manispaa zimepanda jumla ya miti 10,747 katika maeneo ya wazi, mabondeni, mashuleni na pembezoni mwa barabara. Pia usafi umefanyika kwenye maeneo ya mifereji, masoko na fukwe. Shuguli hizi zimeambatana na ukaguzi wa vifaa vya makampuni ya usafi na uhamasishaji wa wananchi katika masuala ya uhifadhi na usafishaji wa mazingira yanayowazunguka. Kwa mkoa wa Dar es Salaam shughuli hizi zilianza tangu tarehe 31/05/2017 na leo hii ndiyo tumefikia siku ya kilele cha Maadhimisho haya.
Ndugu Wananchi,
Licha ya changamoto hizo, zipo pia changamoto za kimazingira ambazo zinatokana na ukiukwaji wa sheria kunakosababishwa na wananchiukiukwaji huo ni kama utupaji taka ovyo, utiririshaji maji machafu, uchimbaji holela wa mchanga, vifusi na kokoto, ukataji miti holela, biashara kwenye maeneo yasiyokuwa rasmi na ujenzi holela katika maeneo hatarishi hususani wa mabondeni na kwenye vyanzo vya maji.
Ndugu Wananchi,
Ili kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya Tabianchi pakiwemo na za Kimazingira, Serikali tumeanzisha miradi mbalimbali katika maeneo mbalimbali ya Halmshauri zetu kwa kutumia mapato ya ndani, wadau wa maendeleo na mifuko ya fedha ya kimataifa kwa uborashaji wa miundo mbinu, miradi mbalimbali na mifumo ya ikologia. Miradi hii inahusha na ujenzi wa kingo za bahari, mifereji ya maji ya mvua, uboreshaji wa barabara, upandaji wa mikoko, ukarabati wa matumbawe, upandaji miti, ukarabati wa mwambao wa bahari, na uthibiti wa uvuvi haramu, Vilevile juhudi zimendelea kwa na kukuza uelewa wa matumizi endelevu ya rasilimali kwa wadau na vikundi vya kijamii, kuhusiana na sekta za kilimo, uvuvi, ufugaji na biashara ili kuimarisha uhifadhi wa mazingira.
Vilevile kupitia kwa wataalam wa mazingira Halmashuri zetu zinawajibika kudhibiti miradi na viwanda chafuzi kwa mazingira, kwa kusimamia tathmini na hakiki za Athari kwa Mazingira, ukaguzi wa viwanda na kuhakikisha miradi yote inayoanzishwa inakuwa na mipango ya kusimamia mazingira. Uhifadhi wa mazingira ukipewa umuhimu unaostahili tutaweza kupambana na uharibifu wa mazingira na kusababisha changamoto zitokanazo na umasikini, maradhi, hali mbaya na duni ya upatikana chakula, makazi duni, maji yasiyo salaama na upatikanaji wa nishati usioridhisha na kusambaa holela kwa mji.
Ndugu wananchi,
Suala la taka ngumu na usafi wa mazingira limekuwa na changamoto katika Mkoa wetu. Inakadiriwa kwa sasa Mkoa huu una watu zaidi ya milioni 5 na viwanda vikubwa na vidogo vipatavyo 1,885 ambapo kwa pamoja huzalisha taka tani 4,500 kwa siku, takiribani asilimia 50 ya taka zinazo zalishwa huzolewa na kupelekwa kwenye kituo cha kutupia taka (dampo) na asilimia 50 hubaki mitaani kutokana na uwezo mdogo wa Halmashauri. Inakadiriwa kwamba asilimia 70 ya taka zinazozalishwa ni za kuoza (organic waste) ambazo zina athari kubwa zikiachwa kwenya mazingira. Kutokana na hali hii mkoa unao mpango wa kuanzisha kiwanda cha kuchakata taka na kuwa mbolea ambapo wakulima wa Dar es salaam watajengewa uelewa na kuhamasishwa kutumia mbolea inayotokana na taka hizo na mpango huu utapunguza kiwango cha taka zinazobaki mitaani.
Ndugu Wananchi
Kwa kuzingatia kauli mbiu ya mwaka huu, ni dhahiri kwamba imebeba ujumbe kamili wa kumuunganisha mwananchi na Mazingira asilia yanayomzunguka (Connecting People to Nature); inatoa mwanya kwa wakazi wote wa Mkoa wetu kutafakari upya kama shughuli wanazozifanya zinazingatia utunzaji wa Mazingira endelevu na yenye tija kwa ajili ya Maendeleo ya sasa na ya baadaye.
Ndugu Wananchi,
Kutokana na changamoto zinazo tukabili nasisitiza kuwa Sheria ya Mazingira, sheria za kisekta na Sheria Ndogo zilizopo zinazohusiana na usafi na utunzaji wa Mazingira zitumike inavyopaswa ili kuondoa utupaji taka ovyo, utiririshaji maji machafu na mchimbaji holela wa mchanga, vifusi na kokoto, ukataji miti holela, biashara kwenye maeneo yasiyokuwa rasmi na ujenzi holela hususani wa mabondeni na kwenye vyanzo vya maji.
Nasisitiza kuwa ni wajibu wa Watendaji wote waliopewa dhamana na Serikali wanawajibu wa kulinda na kusimamia usafi na utunzaji wa mazingira katika maeneo yao. Natoa wito kwa wananchi wote wa Mkoa wa Dar es Salaam kutoa ushirikiano wa dhati ili kuunga mkono juhudi na mikakati ya kutunza na kuhifadhi mazingira kwani mazingira ndio urithi kwa vizazi vya baadaye.
Mwisho naomba Wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam kuunga Mkono juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano za kuifanya nchi yetu kuwa nchi ya viwanda; kuongoza mapambano dhidi ya madawa ya kulevya; kuhimiza usafi wa mazingira na kuondoa utoroshaji wa rasilimali za nchi.
Nachukua nafasi hii kuwashukuru wadau wote wa kutoka taasisi za umma na za binafsi mnaoshirikiana nasi katika masuala yote yanayohusiana na mazingira. Ninawaomba mwendelee kuiunga mkono Serikali yenu kwa kuyatunza, kuyalinda na kuyahifadhi Mazingira yetu.
Kwa mara nyingine nawashukuru wananchi wote, kwa kujitokeza kwa wingi siku hii ya leo kwa ajili ya kuadhimisha siku hii muhimu duniani
ASANTENI KWA KUNISIKILIZA
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa