Katibu Tawala Mkoa,
Waheshimiwa Mameya wote
Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa
Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa
Mratibu wa Elimu wa Mkoa
Mwakilishi kutoka TAMISEMI
Mwakilishi wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,
Waheshimiwa Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Wilaya,
Waganga Wakuu wa Wilaya
Viongozi wa dini mbalimbali
Kamati ya Afya ya msingi
Ndugu Wanakamati,
Awali ya yote,napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima na afya njema na kutuwezesha sote kuwa hapa siku ya leo. Pili napenda kuwashukuru kujumuika nanyi katika tukio hili muhimu la mkutano wa Kamati ya Afya ya Msingi ngazi ya Mkoa kuzungumzia chanjo mpya ya mlango wa kizazi katika Mkoa wetu.Pia, nachukua fursa hii kuwapongeza wote ambao mmejumuika hapa na ushiriki wenu katika mkutano huu muhimu.
Ndugu Wanakamati
Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watotokwa kushirikiana na wadau wa chanjo,nimeambiwa mmeazisha chanjo mpya ya kuwakinga na ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi wasichana wenye umri wa miaka 14 kuanzia mweziApril,2018 nchi nzima. Serikali imeamua kuanza kutoa chanjo hii kwasababu saratani ya mlango wa kizazi ndiyo inayoongoza kwa kuua wanawake wengi ukilinganisha na saratani nyingine hapa Tanzania.
Ndugu wanakamati,
Saratani ya mlango wa kizazi inachangiwana vitu vingi ikiwemo kuanza kujamiana katika umri mdogo,kuwa na wapenzi wengi,kuwa na ndoa za mitala,kuzaa watoto wengi, na uvutaji wa sigara.Dalili za saratani ya mlango wa kizazi mara nyingi hujitokeza ikiwa imeshasambaa mwilini.Zifuatazo ni baadhi ya dalili za saratani mfano; kutokwa damu ya hedhi bila mpangilio,kutokwa damu baada ya kujamiiana,maumivu ya mgongo, miguu na/au kiuno,kuchoka, kupungua uzito, kupungukiwa au kukosa hamu ya kula,kutokwa na uchafu wa rangi ya kahawia au wenye damu kwenye uke,maumivu ya miguu au kuvimba miguu.
Dalili mbaya zaidi zinazoweza kujitokeza ni pamoja na kuishiwa damu, figo kushindwa kufanya kazi, kupatwa na fistula, na uvimbe wa tezi.
Ndugu Wanakamati
Lengo hasa la kuanzisha chanjo hii ni kuwakingamabinti zetu na madhara yanayoweza kuwapata ambayo yanasababisha vifo kwa wanawake, na hivyo, uanzishwaji wa chanjo hii utaboresha Afya ya Wakazi wa mkoa wetu na Watanzania kwa ujumla.Walengwa wa chanjo hii kwa mwaka huu wa 2018 ni wasichana wote wanaotimiza miaka 14, ambao kwa mkoa wetu tunatarajia kuchanja wasichana wasiopungua elfu ishirini na nne na tisini na saba ifikapo Disemba 2018(24,097).
Ndugu Wanakamati,
Tunapaswa kujua namna ya kujikinga na Saratani ya mlango wa kizazi.Njia yakwanza ni kupata chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi, kutokufanya ngono katika umri mdogo, kuepuka kubeba mimba katika umri mdogo, kuwa na mwenzi mmoja mwaminifu, kutumia kondomu na kuepuka uvutaji wa sigara. Njia ya pili niKufanya uchunguzi wa kina ili kubaini dalili za awali na kupata matibabu stahiki mapema. Na njia ya tatu, kupata matibabu maalum kwa mtu ambaye tayari amepata saratani ya mlango wa kizazi.
Ndugu Wanakamati,
Napenda pia niwataarifu mkakati uliotumika katika utoaji wa chanjo hii. Kutokana na uzoefu uliopatikana wakati wa majaribio ya utoaji wa chanjo hii uliofanyika Mkoani Kilimanjaro,chanjo hii itatolewa katika utaratibu wa kawaida katika vituo vyetu vya kutolea huduma za chanjo, baadhi ya shule zitakazochaguliwa, na baadhi ya maeneo katika jamii ambapo zitatolewa kwa njia za huduma za mkoba.Huduma hizi zitatolewa bila malipo katika vituo vya kutolea huduma za afya vya serikali na binafi.Wizara yetu kwa kushirikiana na wadau tumejipanga vizuri kuhakikisha watoto wetu wanaondokana na tatizo hili.
Ndugu Wanakamati,
Napenda kuipongeza Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na wadau mbalimbabali katika jitihada za kuboresha afya ya mabinti zetu hapa Nchini ikiwepo kupunguza vifo vitokanavyo na saratanikwa kuanzisha chanjo dhidi ya ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi.Tunafahamu kuna changamoto nyingi katika mapambano dhidi ya saratani. Tunajaribu kukabiliana na changamoto zilizopo, ili kusimamia na kuboresha Afya ya Wakazi wa Mkoa wetu wa Dar es salaam.
Ndugu Wanakamati,
Napenda kusisitiza katika Mkoa wetu kuwahakikishia kwamba tutajitahidi kadri ya uwezo wetu kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha kuwa chanjo zote zinakuwepo vituoni muda wote.
Nchini Tanzania, saratani ya mlango wa kizazi ni ya kwanza kwa vifo ikifuatiwa na saratani ya matiti. Saratani hizi mbili kwa pamoja husababisha zaidi ya asilimia 50 ya vifo vyote vya wakina mama vitokanavyo na saratani. Idadi hii ni kubwa sana, hivyo juhudi na ushirikiano zaidi vinahitajika katika kupunguza vifo hivi. Aidha takwimu zinaonesha kuwa ni asilimia 5 tu ya fedha za saratani duniani zinazotolewa katika nchi za kusini mwa jangwa la sahara. Hivyo basi, hatuna budi kutumia vyanzo vyetu vya mapato vya ndani pamoja na kushirikiana na wadau mbalimbali katika kutoa huduma za chanjo.
Ndugu Wanakamati,
Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru wadau wetu wa huduma za chanjo likiwemo Shirika la Gavi,Pamoja na serikali yetu kuwa mstari wa mbele kufadhili huduma za chanjo ikiwemochanjo ya kuzuia dondakoo, kifaduro, homa ya uti wa mgongo,homa ya ini, pepopunda,Nimonia,kuzuia kuhara, Surua na Rubella, na sasa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi.
Ndugu Wanakamati,
Pamoja na kudhibiti magonjwa mengine yanayozuilika kwa chanjo, Tanzania imeendelea kutokuwa na wagonjwa wa polio kwa zaidi ya miaka 18. Mwaka 2015 novemba, Tanzania ilitangazwa kuwa miongoni mwa nchi zilizothibitika kutokuwa na ugonjwa huu; pia Tanzania imeishatangazwa kuwa ni nchi iliyothibitishwa kutokuwa na ugonjwa wa pepopunda kwa watoto wachanga tangu mwaka 2011.
Ombi langu kubwa kwenu kama Kamati ya Afya ya Msingi ya Mkoa ni kusimamia na kuratibu shughuli na kazi ya utoaji wa chanjo inayoendelea katika Halmashauri zetu zote tano, kuona kuwa idadi iliyokusudiwa ta wasichana wanaopata chanjo hii inafikiwa.Wengi wetu tumetembelea Ocean Road na kuona jinsi jamaa zetu wanavyopata mateso makali. Kuwahimiza walengwa wote kufika katika kituo cha kutolea huduma za chanjo naakina mama nao wajitokeze kwa wingi iliwaweze kufanyiwa uchunguzi dhidi ya ugonjwa wa sratani ya mlango wa kizazi kwani huduma hii inatolewa bila malipo.kwa kufanya hivyo kutasaidia kuwakinga na magonjwa na vifo, hii itaiwezesha Serikali kutumia fedha ambazo zingetumika kugharamia matibabu zitumike katika miradi mingine ya maendeleo. Kwa kuwa chanjo ni uwekezaji katika uchumi wa Taifa, serikali hutoa chanjo hizi bila malipo katika vituo vyote vinavyotoa huduma za chanjo vikiwemo vya serikali, binafsi, Mashirika ya dini na yasiyo ya kiserikali.
Ndugu Wanakamati,
Napenda kuchukukua fursa hii kuwashukuru tena wadau mbalimbali waliochangia katika kufanikisha utoaji bora wahuduma za chanjo hapa nchini.Natoashukuranizanguzadhatikabisakwashirika la GAVI,Shirika la afyaulimwenguni WHO.Shirika la kuhudumiawatoto UNICEF, CHAI, JSI, PATH, AMREF, JHPIEGO pamoja na wadau wengine kwa misaada yao ambayo imeweza kutufikisha hapa tulipo.
Ndugu wanakamati
Ninachukua fursa hii kuomba Kamati hii ushirikiano wenu wa kusaidia kupeleka ujumbe huu katika kila hadhara na mikutano mbalimbali kuweza kueleza juu ya uanzishwaji wa chanjo hii na ushiriki wa jamii ili kuhakikisha zoezi la chanjo hii unapata Baraka zote, na kamwe kusiwe na mtu wa kuzuia watoto wetu ambao ni taifa la kesho kutopata kinga hii muhumu ya kuzuia madhara makubwa yanayoweza kuwapata hapo baadae.Kama wengi wetu tunavyofahamu kuwa ugonjwa wa saratani hujitokeza baadae sana wakati wa kuelekea utu uzima.
Wazazi/Walezi, wahakikishe kuwa watoto ambao wamefikisha umri wa miaka 14 wanaenda katika vituo vya kutolea huduma za chanjo ikiwemo vituo vya Afya, shule na baadhi ya maeneo katika jamii yaliyopangwa kutumika kwa huduma ya utoaji wa chanjo kama huduma ya mkoba (out rech services).
Akina mama pia wajitokeze kwa wingi ili wafanyiwe uchunguzi wa awali juu ya saratani ya mlango wa kizazi.
Tuanaomba ushirikiano wa wadau na wananchi wote kwa ujumla ili tuweze kufikia lengo letu la kuhakikisha kila mwananchi anakuwa na afya bora
Naomba nihitimishe kwa kuwahakikishia wananchi kuwa chanjo zinazotolewa katika vituo vyetu ni salama, hutolewa na wataalamu wenye uzoefu mkubwa waliobobea katika fani hii kwa muda mrefu.
Mwisho napenda niwashukuru wote kwa kufika katika mkutano huu muhimu.
Baada ya kusema hayo naomba kutangaza kuwa mkutano wetu wa Kamati ya Afya ya Msingi ngazi ya Mkoa unaohusu chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi umefunguliwa rasmi.
ASANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa