HOTUBA YA KATIBU TAWALA WA MKOA WA DAR ES SALAAM
BIBI THERESIA MMBANDO KWENYE KIKAO CHA KAMATI YA UCHAGUZI WA WANAFUNZI WA KUJIUNGA KIDATO CHA KWANZA MWAKA 2018 TAREHE 8 DESEMBA, 2017 KWENYE
UKUMBI WA ARNATOUGLO – MNAZI MMOJA
Ndugu Katibu wa Kamati;
Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya;
Waheshimiwa Wastahiki Mameya wa Manispaa;
Waheshimiwa Wabunge;
Ndugu Mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI;
Ndugu Wajumbe wa Kamati ya Uendeshaji Mitihani Mkoa;
Waheshimiwa Wenyeviti wa Kamati za Huduma za Uchumi, Afya na Elimu wa Halmashauri za Manispaa;
Ndugu Wakurugenzi wa Manispaa;
Ndugu Makatibu Tawala wa Wilaya;
Ndugu Wawakilishi wa Wakuu wa Shule za Serikali na zisizo za Serikali;
Ndugu Wawakilishi wa Asasi mbalimbali;
Kamati ya Sekretarieti ya Uchaguzi;
Waandishi wa Habari;
Mabibi na Mabwana;
Ndugu wajumbe na Wageni waalikwa;
Awali ya yote nichukue fursa hii kuwakaribisha Wajumbe na waalikwa wote katika kikao hiki cha Kamati ya Mkoa cha Uchaguzi wa Wanafunzi wa Kujiunga na Kidato cha Kwanza mwaka 2018.
Ndugu Wajumbe na Wageni waalikwa;
Kama alivyoeleza Katibu wa kikao, agenda kuu ya kikao ni ya kuwachagua wanafunzi wa Mkoa wa Dar es Salaam waliofanya na kufaulu Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi mwaka 2017 watakaojiunga na Kidato cha Kwanza mwaka 2018. Mtakumbuka kuwa tulikutana kwa mara ya mwisho tarehe 28 Novemba, 2016 katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kufanya kazi kama hii. Natumia nafasi hii kuwapongeza kwa kazi nzuri mliyoifanya tangu ulipofanyika uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na Kidato cha Kwanza mwaka 2017. Hatujapokea malalamiko juu ya uchaguzi ule, hivyo mlikuwa makini katika kutenda haki na nategemea hata mwaka huu tumefanya vizuri zaidi.
Ndugu Wajumbe na Wageni waalikwa;
Kabla ya kufanya kazi ya kuchagua wanafunzi watakaojiunga Kidato cha Kwanza mwaka 2018, napenda kueleza machache kuhusiana na mwenendo wa ufaulu wa Mkoa wetu kwenye Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi kuanzia mwaka 2013 hadi mwaka 2017 kama ifuatavyo:-
Ndugu Wajumbe na Wageni waalikwa;
Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imepata ufaulu wa juu zaidi ya Manispaa nyingine sio tu katika Mkoa wetu bali kwa nchi nzima. Halmashauri hiyo imepata asilimia 93.02 na hivyo kushika nafasi ya kwanza Kitaifa ikifuatiwa na Manispaa ya Ilala (Mjini) asilimia 92.46 (nafasi ya 4 Kitaifa) kisha Kigamboni iliyopata asilimia 91.10 (nafasi ya 7 Kitaifa) ikilinganishwa na matokeo ya mwaka jana 2016 ambapo Kinondoni walipata asilimia 84.20, Ilala walipata asilimia 83.43 na Temeke asilimia 81.70.
Matokeo hayo mazuri yametokana na dhamira ya dhati ya kuhakikisha ufaulu unapanda uliyofanywa kwa ushirikiano wa Wadau mbalimbali wakiwemo wanafunzi wenyewe, walimu, kamati za shule, wazazi, maafisa elimu na viongozi wa ngazi zote.
Nachukua nafasi hii kwa namna ya pekee kabisa kuwapongeza sana walimu, wanafunzi, viongozi na wadau wote kwa usimamizi na ufuatiliaji wenye ufanisi uliotuletea matokeo haya. Tumeweza kupata Wilaya tatu za kinondoni, Ilala Mjini na Kigamboni katika Wilaya kumi bora Kitaifa huku Kinondoni ikishika nafasi ya kwanza Kitaifa. Hongereni sana tuzidi kuimarisha utendaji ili tuendelee kubaki kwenye nafasi hiyo.
Katika kikao hiki, wanafunzi wanaopendekezwa kuchaguliwa kujiunga na Kidato cha Kwanza mwaka 2018 ni 58,573 sawa na asilimia 87.82 ambapo wavulana ni 28,103 na wasichana 30,470. Hakuna wanafunzi waliofaulu ambao hawajapangiwa shule.
Ndugu Wajumbe na Wageni waalikwa;
Uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na Kidato cha Kwanza mwaka 2018 umezingatia mwongozo uliotolewa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa Makatibu Tawala wa Mikoa wenye Kumb. Na. DC.292/507/01/99 wa tarehe 1/11/2017 ambao unaelekeza kuwa wanafunzi waliofaulu ni wale waliopata alama 250 hadi 100. Kwa hiyo katika Mkoa wa Dar es Salaam wanafunzi 58,573 wamefaulu wakiwemo wavulana 28,103 na wasichana 30,170 ambao wamechaguliwa kujiunga na Kidato cha Kwanza mwaka 2018.
Ufuatiliaji uliofanywa na uongozi wa Mkoa umebaini kuwa wanafunzi wengi wanaofaulu kutoka katika Shule za Msingi za mjini wakipangwa shule za vijijini huwa wanashindwa kuhudhuria mfululizo shuleni kutokana na umbali na gharama za usafiri na wengi wao huacha shule.
Ahadi zimekuwa zikitolewa na Halmashauri za Manispaa kuwawekea utaratibu maalum wa usafiri na ujenzi wa daharia (Hostel) wanafunzi hawa zimekuwa hazitekelezwi Mwaka jana 2016 jumla ya nafasi 1,246 katika shule zilizo pembezoni ziliachwa wazi kutokana na umbali uliopo kati ya shule ya msingi mwanafunzi aliyosoma na shule ya sekondari aliyopangiwa, mwaka huu jumla ya nafasi 4,685 zimeachwa wazi. Hivyo ikiwa kuna mzazi au mlezi atakayekuwa na uhakika wa kupata sehemu ya kuishi ama usafiri wa uhakika wa mwanae kwenda shuleni atapewa nafasi baada ya kujaza fomu maalum (SS 4). Nawasihi wajumbe kuanza kutekeleza wazo la shule za pembezoni kuwa na daharia (hostel) ili kuondoa changamoto hii ya kubaki kwa nafasi wazi.
Ndugu Wajumbe na Wageni waalikwa;
Tunayo changamoto ya nafasi wazi 4,685 ambapo Ilala ni 887, Kigamboni 590, Kinondoni 1,718 na Ubungo 1,490 na uhaba wa vyumba vya madarasa 291 ambavyo vinasababisha wanafunzi 11,640 kuombewa kibali cha kusoma kwa utaratibu wa “double shift” kwa shule 20 za Manispaa ya Ilala kwa wanafunzi 5,515 ambao wanahitaji vyumba vya madarasa 138, Manispaa ya Temeke shule 20 kwa wanafunzi 5,600 ambao wanahitaji vyumba vya madarasa 140 na Manispaa ya Ubungo shule 6 kwa wanafunzi 525 ambao wanahitaji vyumba vya madarasa 13.
Pawepo na mkakati wa kujenga daharia “hostels” kwenye shule zilizo pembezoni ili wanafunzi waweze kulala huko au papatikane maeneo katikati ya Jiji kwa ajili ya kujenga shule, Mkoa wa Dar es Salaam una jumla ya Kata 102, kati ya hizo Kata 21 hazina Shule za Sekondari za wananchi. Kwa mfano Manispaa ya Kinondoni, Kata 3 ambazo ni Magomeni, Kinondoni na Tandale. Katika Manispaa ya Temeke kuna Kata 5 zisizo na shule ambazo ni Chang’ombe, Makangarawe, Mbagala, Kilungule na Kibondemaji. Aidha, katika Manispaa ya Kigamboni Kata moja ya Kigamboni haina shule. Pia Manispaa ya Ilala ina Kata 12 ambazo ni Upanga Mashariki, Upanga Magharibi, Kisutu, Kivukoni, Mchafukoge, Kariakoo, Buguruni, Mnyamani, Liwiti, Bonyokwa, Ukonga na Kipunguni hazina shule ya Sekondari. Katika Kata ya Kiwalani shule imejengwa eneo la maji (bwawa) hali iliyosababisha wanafunzi kutoka maeneo ya Kata za jirani kutopelekwa mahali hapo.
Niwapongeze Wajumbe wa Manispaa ya Kinondoni ambao wamechukua hatua kwa mwaka huu kujenga shule katika Kata 2 za Mzimuni na Mbezi Juu. Hali kadhalika Wajumbe wa Manispaa ya Ubungo kwa hatua ya kujenga shule katika Kata ya Kimara ambazo awali hazikuwa na shule za Sekondari. Jitihada hizi zinapaswa kuigwa na Halmashauri zingine ili kuondokana na changamoto za wanafunzi kupangwa mbali na maeneo wanayotoka au kuishi.
Ndugu Wajumbe na Wageni waalikwa;
Pamoja na jitihada kubwa zinazofanyika katika kupandisha ufaulu wa wanafunzi mashuleni, bado tunayo changamoto ya idadi kubwa ya wanafunzi kupangwa katika shule na kusababisha wanafunzi kusoma kwa zamu kwa maana ya “double shift”. Jumla ya wanafunzi 11,640 waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha kwanza mwaka 2018 wameombewa kibali cha kusoma kwa mpango huo. Wajumbe wa Kamati hii ya Uchaguzi Mkoa yafaa sasa tuhusike kikamilifu katika kupanga mbinu na mikakati bora na endelevu ya kuondoa changamoto ya wanafunzi kusoma kwa ‘double shift’ katika Mkoa wetu. Suala hili tumelizungumza mara nyingi katika vikao mbalimbali na mwaka huu tatizo limeongezeka zaidi lakini hadi leo hii hakuna utatuzi wa kudumu wa jambo hili. Hivyo, sasa tuweke malengo yanayotekelezeka ili tuondokane na changamoto hii kwa miaka ijayo.
Aidha kibali kilichoombwa cha wanafunzi kusoma kwa zamu katika shule 46 (Ilala shule 20, Temeke shule 20 na Ubungo shule 6) tumetoa ahadi kwamba hadi mwezi Machi 2018 ambapo jumla ya madarasa 291 yanayohitajika yatakuwa yamekamilishwa (madarasa Ilala madarasa 138, Temeke madarasa 140 na Ubungo madarasa 13). Tutahitaji kupata mpango wa utekelezaji na taarifa ya utekelezaji wa ahadi hiyo kutoka katika Halmashauri hizo zenye upungufu huo na ufuatiliaji utakuwa ukifanyika kila baada ya mwezi mmoja.
Ndugu Wajumbe na Wageni waalikwa;
Mwisho, napenda kumalizia kwa kuwatakia kikao chema chenye ufanisi, kila mmoja wetu atoe maoni yake na ashiriki kikamilifu katika kushauri namna bora ya kuboresha utoaji wa huduma ya elimu katika Mkoa wetu. Nachukua nafasi hii pia kuwatakia kheri ya Krismas na Mwaka Mpya 2018 uwe wenye mafanikio makubwa kwetu na Watanzania wote. Baada ya kusema hayo, sasa natamka rasmi kuwa kikao cha uchaguzi wa wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2018 nimekifungua.
Theresia Mmbando
KATIBU TAWALA MKOA
DAR ES SALAAM
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa