RC Albert Chalamila wa katikati akiwa katika picha ya pamoja na wataalam wa Afya Mkoa na Wizara ya Afya ofisini kwake mara baada ya kuongea na waandishi wa Habari mapema leo
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Albert Chalamila leo Oktoba 30 ametoa taarifa kwa umma kupitia vyombo vya habari kuhusu maadhimisho ya wiki ya kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza Kitaifa Ofisi kwake Ilala Boma ambapo amesema Mkoa huo umepata bahati ya kuchaguliwa kuwa mwenyeji wa maadhimisho hayo.
RC Chalamila ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa huo na Mikoa Jirani kutumia fursa hii adhimu kujitokeza kwa wingi, kwa kuwa maadhimisho hayo mwaka huu 2023 yatatanguliwa na Kongamano la kisayanzi linalotarajiwa kufanyika katika ukumbi wa mikutano JNICC kuanzia tarehe 1-3 Novemba 2023, Mgeni Rasmi atakuwa Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa ambapo wataalam mbalimbali wa Afya kutoka katika Taasisi za Elimu na Utafiti watajadili mikakati mbalimbali ya kukabiliana na tatizo hilo " Wananchi na wadau mbalimbali mliopo katika Mkoa wa Dar es Salaam na nje ya Mkoa mjitokeze kushiriki Kongamano hili muhimu". Alisema RC Chalamila
Aidha RC Chalamila amesema baada ya Kongamano la kisayanzi Wananchi watapata fursa ya kupata huduma za upimaji Afya bure pamoja na elimu ya kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza, huduma hizo zitatolewa kwenye viwanja vya Mnazimmoja Wilaya ya Ilala kuanzia Novemba 11, hadi 18, 2023, " Wananchi jitokezeni kwa wingi katika maadhimisho hayo ikiwa ni pamoja na kujitokeza kupima afya zao Bure , Kinga ni Bora Kuliko Tiba" alisisitiza Mhe Chalamila
Tafiti nyingi zilizofanyika zinaonesha magonjwa yasiyoambukiza yanatokana na mabadiliko ya mtindo wa maisha katika Jamii, takwimu zinaonesha uwepo wa matumizi makubwa ya pombe ambapo asilimia 29.3 ya watu wana matumizi makubwa ya pombe, asimia 15.9 wanatumia tumbaku huku zaidi ya asilimia 97 hawazingatii ulaji unaofaa, vilevile RC Chalamila amemshukuru Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa katika sekta ya Afya ambao una masilahi mapana kwa Umma.
Dkt Rashid Mfaume akifafanua jambo wakati wa mkutano na waandishi wa Habari kuhusu magonjwa yasiyoambukiza.
Kwa upande wa Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt Rashid Mfaume amesema maadhimisho ya mwaka huu yenye kauli mbiu " Usijisahau, Jali Afya Yako wataalam wa Mkoa kwa kushirikiana na Wizara ya Afya wameshajipanga vizuri, ameendelea kutoa rai wananchi kujitokeza kwa wingi ambapo amesema taarifa za kitaalam zinaonesha vifo vinavyotokana na magonjwa yasiyoambukiza hapa nchini vimeongezeka ambapo kila vifo vitatu kimoja kinatokana na magonjwa haya aidha watu wanaopata magonjwa ya shinikizo la juu la damu imeongezeka mara 5 zaidi ndani ya Kipindi cha miaka 40 ambapo kwa sasa kila watu 4 mmoja anatatizo hilo.
Sambamba na hilo ikilinganisha na miaka ya 80 ilikuwa ni mtu mmoja tu mwenye tatizo hilo katika kila watu 20, hali kama hii inaonekana pia katika magonjwa mengine ya Saratani na kiharusi ambapo ongezeko ni kubwa kwa zaidi ya mara 9 ikilinganisha na miaka ya 80
Mratibu wa huduma za seli mundu kutoka Wizara ya Afya Bi. Asteria Mpoto wa kwanza kushoto akitoa ufafanuzi wa namna wizara ya afya ilivyojipanga kuealekea maadhimisho ya wiki ya magonjwa yasiyoambukiza ambayo kitaifa yanafanyika Mkoa wa Dar es Salaam.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa