HOTUBA YA KATIBU TAWALA WA MKOA WA DAR ES SALAAM
NDUGU ABUBAKAR M. KUNENGE ILIYOSOMWA NA AFISA ELIMU WA MKOA NDUGU HAMIS S. LISSU KWENYE KIKAO CHA KAMATI YA UCHAGUZI WA WANAFUNZI WA KUJIUNGA KIDATO CHA KWANZA MWAKA 2019 TAREHE 14 DESEMBA, 2018 - UKUMBI WA
ARNATOUGLO, MNAZI MMOJA
Ndugu Katibu wa Kamati;
Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya;
Waheshimiwa Wastahiki Mameya wa Manispaa;
Waheshimiwa Wabunge;
Ndugu Mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI;
Ndugu Wajumbe wa Kamati ya Uendeshaji Mitihani Mkoa;
Waheshimiwa Wenyeviti wa Kamati za Huduma za Uchumi, Afya na Elimu wa Halmashauri za Manispaa;
Ndugu Makatibu Tawala wa Wilaya;
Ndugu Wakurugenzi wa Manispaa;
Ndugu Wawakilishi wa Wakuu wa Shule za Serikali na zisizo za Serikali;
Kamati ya Sekretarieti ya Uchaguzi;
Waandishi wa Habari;
Mabibi na Mabwana;
Habari za Asubuhi!
Ndugu wajumbe na Wageni waalikwa;
Awali ya yote nichukue fursa hii kuwakaribisha wote katika kikao hiki cha Kamati ya Mkoa cha Uchaguzi wa Wanafunzi wa Kujiunga na Kidato cha Kwanza mwaka 2019.
Ndugu Wajumbe na Wageni waalikwa;
Kama alivyoeleza Katibu wa kikao, agenda kuu ya kikao hiki ni moja ambayo ni ya kuwachagua wanafunzi wa Mkoa wa Dar es Salaam ambao walifanya Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi (PSLE) mwezi Septemba, 2018 watakaojiunga na Kidato cha Kwanza mwaka 2019. Kila mwaka tunafanya mkutano kama huu mara moja ambapo mwaka jana ulifanyika tarehe 8 Desemba, 2017 katika Ukumbi huu wa Arnatouglo kwa lengo kama hili. Natumia nafasi hii kuwapongeza kwa kazi nzuri mliyoifanya kwenye kikao hicho kwani tangu ulipofanyika uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2018 hatujapokea malalamiko juu ya uchaguzi ule, hiyo inaonesha ni kwa namna gani mlikuwa makini katika kutenda haki kwa vijana wetu. Nategemea hata mwaka huu tutafanya vizuri zaidi.
Ndugu Wajumbe na Wageni waalikwa;
Kabla ya kufanya kazi ya kuchagua wanafunzi watakaojiunga Kidato cha Kwanza 2019, napenda kueleza machache kuhusiana na mwenendo wa ufaulu wa Mkoa wetu kwenye Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi kwa miaka mitano iliyopita kama ifuatavyo:-
Ukiangalia takwimu nilizozitaja hapo juu, utabaini kuwa matokeo ya Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi mwaka 2018 yamepanda kwa asilimia 4.44 kutoka asilimia 87.82 mwaka 2017 hadi 92.26 mwaka 2018. Mwaka huu pia Mkoa umeshika nafasi ya kwanza (01) Kitaifa ambayo ilishika mwaka jana 2017. Hongereni sana kwa kubakia kwenye nafasi hiyo.
Ndugu Wajumbe na Wageni waalikwa;
Nafasi hii ya ufaulu inahitaji ufuatiliaji na uhimizaji wa ufanisi wa kazi kwa walimu, wanafunzi wetu, pia wazazi na walezi waelezwe majukumu yao ili wayatekeleze ipasavyo. Wathibiti Ubora wa Shule washirikiane na Maafisa Elimu Msingi na Wakurugenzi wa kila Halmashauri ya Manispaa kuhakikisha kuwa Mkoa wetu unaendeleza hadhi ya ufaulu wa kwanza Kitaifa. Tuondoe dosari ya udanganyifu ambayo imejitokeza kwenye Mkoa wetu mwaka huu kwa baadhi ya shule zisizo za Serikali hali iliyosababisha wanafunzi wa shule hizo kurudia mtihani. Aidha, shule hizo zimefungiwa kuwa Vituo vya Mtihani ya Taifa.
Ndugu Wajumbe na Wageni waalikwa;
Kuhusu asilimia ya wanafunzi ya kujiungana Shule za Sekondari kwa waliofanya mtihani (transition rate) kwa Mkoa ni asilimia 92.259. Katika Manispaa ya Ilala (Mjini) ni asilimia 95.592, Ilala (Vijijini) 90.501, Kinondoni 95.696, Temeke 90.247, Kigamboni 92.227 na Ubungo 89.788. Watahiniwa wote waliofaulu wamepata nafasi ya Kujiunga Kidato cha Kwanza, 2019.
Ndugu Wajumbe na Wageni waalikwa;
Uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2019 umezingatia mwongozo uliotolewa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa Makatibu Tawala wa Mikoa wenye Kumb. Na. DC.297/507/01 wa tarehe 25/10/2018 ulioelekeza kuwa wanafunzi waliofaulu ni wale waliopata alama 250 hadi 100. Kwa hiyo katika Mkoa wa Dar es Salaam wanafunzi 64,861 wamefaulu wakiwemo wavulana 31,232 na wasichana 33,629 ambao watashindania nafasi za kuchaguliwa kwa usawa kwa kuzingatia ufaulu, machaguo na ukaribu wa shule ya sekondari husika.
Ndugu Wajumbe na Wageni waalikwa;
Napenda kuwafahamisha kuwa mwaka huu Serikali imetoa maelekezo kuhusu matumizi ya Fomu za TSM 9 ambazo wanafunzi hujaza kuomba kuendelea na masomo ya Elimu ya Sekondari baada ya kuhitimu Elimu ya Msingi. Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi katika kuandaa, kupiga picha na kuchapisha Fomu za TSM 9 kama nyaraka muhimu za Serikali kwa wanafunzi wa Darasa la Saba nchini kwa kila mwaka.
Ofisi ya Rais – TAMISEMI imebaini kuwepo kwa udanganyifu mkubwa katika matumizi ya TSM 9 za wanafunzi wanaochaguliwa kujiunga na Kidato cha Kwanza ambapo baadhi ya Wakuu wa Shule za Sekondari wasio waaminifu wamekuwa wakizitumia kwa kuwapa wanafunzi ambao hawakufaulu kujiunga Kidato cha Kwanza au walishamaliza Kidato cha Nne kwa kuwasajili upya shuleni au kuwapa uhamisho kwenda shule nyingine za Serikali.
Mnaagizwa kuwa, kuanzia Januari 2019 wanafunzi wote watakaojiunga na Kidato cha Kwanza kwa Shule za Sekondari za Serikali na zisizo za Serikali, kila Mkuu wa Shule anapaswa kuwa na TSM 9 halali ya mwanafunzi husika kama ifuatavyo:
Ndugu Wajumbe na Wageni waalikwa;
Napenda nipongeze juhudi za Serikali yetu na Wadau mbalimbali wa Elimu ambao kwa ujumla wao wamewezesha Mkoa wetu kupiga hatua kubwa kwa kutoa mIchango na huduma mbalimbali katika shule zetu za msingi na sekondari, naomba tuendelee kushirikiana kwa kadri inavyowezekana.
Kuhusu vyumba vya madarasa, vipo vyumba 431 vinavyojengwa/ kukarabatiwa katika shule za sekondari kwa ajili ya maandalizi ya kupokea wanafunzi tutakaowachagua leo.
Ndugu Wajumbe na Wageni waalikwa;
Nawaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri kujipanga kikamilifu kufuatilia maendeleo ya shule zitakapofunguliwa tarehe 07/1/2019 muweze kuona hali halisi ya namna wanafunzi wanavyoripoti shuleni, hali ya wanafunzi katika vyumba vya madarasa, utoshelevu wa madawati na shughuli za ufundishaji na ujifunzaji. Hakikisheni kuwa mipango ya kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza inatekelezwa kama mlivyopanga.
Mwisho, napenda niwatakie kikao chema chenye ufanisi, pia kheri ya Krismas na Mwaka Mpya 2019 uwe wenye mafanikio makubwa kwetu na kwa Watanzania wote. Baada ya kusema hayo, sasa natamka rasmi kuwa kikao cha uchaguzi wa wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2019 nimekifungua.
Asanteni kwa kunisikiliza.
Abubakar M. Kunenge
KATIBU TAWALA MKOA
DAR ES SALAAM
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa