Balozi wa Uingereza nchini Tanzania Bi. Sarah Cooke amemtembelea Ofisini kwake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Paul C. Makonda tarehe 23/05/207 na kufanya nae mazungumzo yenye lengo la kuongeza na kuimarisha Ushirikiano uliopo baina ya Jiji la Dar es Salaam na London nchini Uingereza.
Katika mazungumzo yao Mhe. Paul C. Makonda na Bi. Sarah Cooke wamekubaliana kuongeza kasi ya Ushirikiano baina ya Majiji makubwa mawili ya Dar es Salaam – Tanzania na London nchini Uingereza, makubaliano ambayo yatasaidia kupatikana kwa vifaa vya kisasa vya kuzuia na kupambana na majanga kama vile moto na mafuriko ambapo Mhe. Mkuu wa Mkoa ameomba kupatiwa magari ya kisasa ya shughuli za kuzima moto na uokoaji.
Aidha, Mhe. Mkuu wa Mkoa ameomba kusaidiwa vifaa maalum vya UTAMBUZI wa mifumo ya teknolojia ya Kamera za kisasa zitakazofungwa barabarani kwa ajili ya kusaidia USALAMA wa magari, raia na mali zao mifumo ambayo inafanya kazi katika Jiji la London nchini Uingereza hatua itakayokwenda sambamba na ujengewaji wa UWEZO kwa maofisa wa Polisi wa Mkoa wa Dar es Salaam katika matumizi ya mifumo hii.
Katika kukabiliana na changamoto ya MIGOGORO YA ARDHI Mkoani Dar es Salaam, Mhe. Paul C. Makonda ameomba kusaidiwa kuwajengea uwezo Maafisa Ardhi na Mipango Miji wa Mkoa wa Dar es Salaam katika matumizi ya kisasa ya upimaji na upangaji ardhi, mafunzo ambayo yatakwenda sambamba na upatikanaji wa vifaa vya kisasa vya kupima ardhi jambo litakalosaidia kuondoa KERO YA UPATIKANAJI WA HATI PAMOJA NA VIBALI VYA UJENZI KATIKA MKOA WA DAR ES SALAAM.
Vilevie, katika mazungumzo hayo Mhe. Mhe. Mkuu wa Mkoa na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania wamejadili suala la uanzishwaji wa JIJI LA FIKRA (BRAIN STORMING CENTER) kwa ajili ya kuwakutanisha vijana wabunifu kama ilivyo kwa Tech City ya Uingereza.
Katika kuhitimisha mazungumzo yao Mhe. Mkuu wa Mkoa Paul C. Makonda na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania Bi. Sarah Cooke kwa pamoja wamekubaliana kuzikutanisha timu za wataalamu kutoka London na Dar es Salaam za kukabiliana na majanga haraka iwezekanavyo.
Kwa upande wake Bi. Sarah Cooke amefurahishwa na jinsi Mkuu wa Mkoa anavyopambana na Vita ya Madawa ya Kulevya ambayo imeathiri nguvu kazi kubwa sana katika Jiji la Dar es Salaam na kumuhakikishia kuwa Serikali ya Uingereza inaunga mkono jitihada zote zinazofanywa katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa