Mkoa wa Dar es salaam umedhamiria kuendelea kuimarisha miundombinu ya usafirishaji wa mizigo na watu kwa kujenga barabara bora ili kuufanya Mkoa huo uendelee kuwa kitovu cha uwekezaji na biashara na uendelee kuchangia kwenye pato la nchi kwa asilimia kubwa.
Akizungumza leo Julai 10, 2025 Jijini Dar es Salaam katika maadhimisho ya siku ya Mkoa wa Dar es salaam yaani "Dar es salaam Day" kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mkuu wa wilaya ya Temeke Mhe Sixtus Mapunda amesema Mkoa wa Dar es Salaam ni kitovu cha biashara na unachangia kwenye mapato ya nchi kwa zaidi ya asilimia 17 hivyo Mkoa unaendelea kuimarisha miundombinu ya barabara na madaraja kwa ajili ya usafirishaji, ambapo amesema Mkoa huo unafursa na maeneo mengi kwa ajili ya uwekezaji na biashara kwenye kila wilaya na kwamba ubora wa Mkoa huo unachagizwa na kazi nzuri iliyofanywa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuimarisha Bandari,Usafiri wa reli ya kisasa,uwanja wa ndege pamoja uwepo wa huduma bora za umeme na maji.
Aidha Mhe Mapunda ametoa mchanganuo wa maeneo ya uwekezaji kwa kila wilaya ambapo Wilaya ya Temeke ni maeneo 17,kinondoni maeneo 29 Jiji la Dar es Salaam maeneo 9, kigamboni maeneo 27 na ubungo maeneo maeneo 6 kwa ajili ya uwekezaji.
Kwa upande wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es salaam Bwana Abdul Mhite amesema katika kuimarisha shughuli za biashara na uwekezaji Mkoa huo umekuwa na mikakati mbalimbali ikiwemo kuanzisha mfumo wa biashara saa 24 pamoja na kutoa mikopo ya asilimia 10 kwa wafanyabiashara ambapo zaidi ya vikundi 2000 tayari vimepatiwa mikopo
Maadhimisho ya siku ya Mkoa wa Dar es salaam yamefanyika kwenye viwanja vya SABASABA huku yakijielekeza kwenye mkakati wa kutangaza fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo katika Mkoa wa Dar es Salaam
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa