Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda leo amefanya ziara ya utatuzi wa kero na migogoro ya wakazi wa Buguruni ikiwemo ule wa Wananchi waliovunjiwa nyumba baada ya kujenga ndani ya eneo la reli.
RC Makonda amesema wananchi tunapaswa kuunga mkono juhudi za Serikali za ujenzi wa Reli ya kisasa (Standard Gauge) ambayo inaenda kulifikisha taifa katika uchumi wa kati na kuitangaza Tanzania katika ramani ya Dunia hivyo amewasihi wananchi waliovunjiwa kuwa wavumilivu.
Aidha RC Makonda ameiomba kampuni hodhi ya rasilimali za Reli RAHCO kuangalia uwezekano wa kuwapatia wananchi angalau njia za kupita ili kuwapunguzia mizunguko mirefu.
Katika ziara hiyo RC Makonda amemuagiza Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es salaam Lazaro Mambosasa kumuhamisha kituo kingine Mkuu wa Kituo cha Polisi Buguruni kwa kuwa watu anaowaongoza hawamuamini.
Hata hivyo RC Makonda ametoa siku Saba kwa kigogo wa Bodi ya Mikopo kumkabidhi bajaji kijana alietambulika kwa jina la Jafari Raphael aliyegongwa na gari na kigogo huyo na kupelekea ulemavu wa kukatwa mguu mmoja pasipo kulipwa fidia yoyote na kumfanya kijana huyo kugeuka kuwa mtu wa kuomba misaada huku kigogo huyo akiendelea kula maisha na familia yake.
Pamoja na hayo RC Makonda amepatia ufumbuzi kero ya muda mrefu iliyokuwa ikiwakabili Umoja wa Madereva wa daladala Buguruni Chama waliokuwa wamezuiwa kuegesha magari eneo la Buguruni station ambapo RC Makonda amewaagiza madereva hao kurudi katika eneo hilo.
Miongoni mwa kero zilizotolewa na wakazi wa Buguruni ni pamoja na tozo kubwa ya uchafu, polisi jamii,ukamataji wa watu, watu kubambikiziwa kesi, migogoro ya mirathi na watu kudhulumiwa ambapo RC Makonda amezipatia majibu kero hizo papo kwa papo kwa kupigia simu kwa walengwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa