Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka Viongozi wa ngazi zote kuongeza nguvu katika utekelezaji wa Sera, Sheria, Mikakati na Miongozo katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira.
Makamu wa Rais ameyasema hayo wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ambayo kitaifa imefanyika jijini Dar es Salaam kwenye Viwanja vya Mnazi mmoja.
“ Ni muhimu, mipango ya maendeleo katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira ili nchi yetu iwe na maendeleo endelevu” alisema Makamu wa Rais.
Makamu wa Rais amesema kazi ya kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa Uhifadhi wa Mazingira inahitaji ushirikiano wa wadau wote kwa ngazi zote.
Ameongeza kuwa watanzania wanapaswa kuelewa athari zitokanazo na ukataji wa miti kiholela na kuhakikisha wanakuwa walinzi wa kwanza wa Mazingira hayo.
Amezitaja athari hizo kuwa ni kukimbiza wanyama, kupoteza matunda ya asili, kuharibu makazi ya wadudu wenye kazi mbalimbali, kuharibu misitu inayotusaidia kunyonya joto au hewa ukaa na bahari kuingia eneo la makazi ya watu.
Maadhimisho ya Kimataifa yanafanyika India katika mji wa New Delhi yakibeba ujumbe wa kuhimiza kupunguza uchafuzi wa Mazingira kutokana na matumizi ya bidhaa za plastiki (Beat Plastic Pollution) lakini hapa nchini Kitaifa ujumbe wa maadhimisho ni “Mkaa Gharama: Tumia Nishati Mbadala”.
Awali, Makamu wa Rais alizindua ukuta wa bahari uliopo kwenye barabara ya Barack Obama wenye urefu wa mita 920, ukuta huo ambao umejengwa kuzuia bahari kuingia nchi kavu unakadiriwa kuwa na maisha kati ya miaka 70 mpaka 100 kutoka sasa.
Makamu wa Rais amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kujenga uchumi wa Viwanda na zipo faida nyingi za hifadhi na usimamizi zitakazotokana na Tanzania kuwa na Viwanda.
Akitoa Salamu za Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Paul Makonda ametangaza kuanza kwa oparesheni kabambe ya kuwakamata na kuwatoza faini wachafuzi wa Mazingira kuanzia July Mosi kwa lengo la kuhakikisha jiji linakuwa kwenye Hali ya usafi kama majiji mengine ulimwenguni.
RC Makonda amesema ameandaa vijana zaidi ya 4,000 kutoka Jeshi la kujenga Taifa JKT ambao watafanya kazi ya kuwakamata watupaji wa taka barabarani na mitaani.
Vijana hao 4,000 ni wale waliomaliza mafunzo ya JKT na hawana kazi ambapo RC Makonda ameamua kuwachukuwa kwa ajili ya kufanya kazi hiyo na kwenye kiasi cha faini watakazo watoza wachafuzi wa mazingira 40% itaenda kwa vijana hao na 60% itaingizwa Serikalini.
Aidha RC Makonda amesema hawezi kukubali kuona Jiji linakuwa kwenye hali ya uchafu wakati ipo sheria ya mwaka 2004 inayotoa mamlaka ya kuwawajibisha wananchi wenye tabia kuchafua mazingira kwa makusudi.
Itakumbukwa kuwa kila mwaka viongozi wamekuwa wakihimiza usafi na hata alipokuja Rais Barack Obama miaka kadhaa iliyopita barabara zilipigwa deki na alipoondoka uchafu ukaendelea na hivi karibuni Rais John Pombe Magufuli alifanya usafi Kama sehemu ya kuhimiza usafi lakini bado watu wamekaidi, pia ulianzishwa utaratibu wa usafi kila jumamosi watu wasifungue maduka hadi wafanye usafi lakini bado pia wamekaidi jambo ambalo RC Makonda ameamua sasa kuja na mkakati wa kuwatumia vijana wa JKT wasiokuwa na kazi kufanya jukumu la kuwakamata wachafuzi wa mazingira.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa