Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam Omar Said Kumbilamoto na Mstahiki Meya Park Heong Joon, Meya wa Jiji la Busan la Korea Kusini wametia saini Mkataba wa kuwa na Uhusiano wa Kidugu (Sistership Relations) baina ya Jiji la Dar es Salaam na Jiji la Busan.
Utiaji saini umefanyika Jijini Busan Korea Kusini tarehe 15 Juni 2023 kwenye Hoteli ya Western Josun.
Jiji la Busan ni la pili kwa ukubwa hapa Korea. Bajeti yake kwa mwaka ni Dola bilioni 10 sawa na Trilioni 23 za kitanzania, ambayo ni nusu ya bajeti ya nchi yetu. Jiji hili lina mahusiano na majiji makubwa 23 katika nchi 26 duniani. Barani Afrika lina mahusiano na majiji ya Western Cape (South Africa), Rabat (Morocco) na Algiers (Algeria).
Jiji la Busan ndio lenye bandari ya lojistiki ya pili kwa ukubwa duniani na bandari ya tano kwa ukubwa ya makontena duniani. Ndio jiji lenye viwanda vya ujenzi wa meli nchini Korea, sekta ya uvuvi na viwanda vya uvuvi. Pia ni jiji la pili kwa sekta ha filamu nchini Korea. Ndio jiji linalotarajiwa kuwa mwenyeji wa Maonyesho ya Biashara ya Dunia (World Expo) iwapo watashinda kinyang'anyiro cha kuwa wenyeji kwa mwaka 2030.
Kufuatia mazungumzo ya awali na katika kuonyesha nia njema, Jiji la Busan tayari limesaini MoU na Bodi ya Filamu nchini kwa ajili ya kusaidia uendelezaji wa sekta ya filamu.
Pichani ni Viongozi wa Jiji la Busan na Dar es Salaam wakionesha nakala za Mikataba waliyotia Saini kuanzisha rasmi ushirikiano wa Kidugu
Baada ya utiaji saini, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mheshimiwa Albert Chalamila aliyeongoza Ujumbe wa Jiji la Dar es Salaam kwenye ziara ya Siku 4 nchini Korea ameelezea hatua hiyo kuwa ya kimkakati itakayofungua fursa mpya za ushirikiano baina ya Majiji yetu Mawili kwenye sekta muhimu za Maendeleo, Biashara, Uchumi na Ustawi wa Jamii
Akizungumzia kuhusu Mkataba wa Ushirikiano uliosainiwa Meya Park wa Jiji la Busan ameeleza kuwa Jiji lake Lipo tayari kushirikiana na Jiji la Dar es Salaam kwenye kujengeana uwezo, kupeana fursa za mafunzo kwa watumishi, ujenzi wa miradi ya maendeleo, uboreshaji wa miundombinu, nishati, sanaa, filamu, udhibiti wa taka na utunzaji wa mazingira
Pichani ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mheshimiwa Albert Chalamila, Meya wa Jiji la Dar es Salaam Omar Said Kumbilamoto, Bw. Amani Ibrahim Mafuru na Bi Theresia Dennis Mwakasungula wa Mamlaka ya Jiji la Dar es Salaam wakiwa na Afisa Ubalozi wa Tanzania nchini Korea Bwana Abilah Namwambe wakiwa kwenye picha ya pamoja na uongozi wa Mamlaka ya jiji la Busan
Akiwa Korea Mheshimiwa Chalamila na ujumbe wake wamezuru Taasisi mbalimbali za Jiji la Busan kujionea utendaji kazi na uratibu wa majukumu mbalimbali ya kimaendeleo
Akizungumzia kuhusu Ushirikiano huu Bw. Namwambe Afisa Ubalozi wa Tanzania Korea Kusini ameeleza kuwa hatua hii ni matunda ya juhudi za Ubalozi za kuhamasisha na kukuza ushirikiano wa taasisi za serikali, sekta binafsi na kukuza ushirikiano wa watu na watu baina ya Tanzania na Korea ili kurahisisha utekelezaji wa sera ya Diplomasia ya Uchumi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa