JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA - OFISI YA WAZIRI MKUU - TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA      
 
     
 
     
MAJI
 
Maji [ Nyumbani ]
 
 
 

UTANGULIZI

 
Maji ni rasilimali muhimu kwa maisha ya viumbe vyote na mendeleo ya kiuchumi na kijamii. Kiwango cha maendeleo ya jamii yoyote, ubora wa afya na wa mazingira vinategemea kuwepo kwa maji yakutosha na yenye ubora unaotakiwa.

Wingi wa maji yanayofaa kwa matumizi mbalimbali una kikomo. Kutokana na ukomo wa wingi wa maji yenye ubora na umuhimu wake kwa maisha ya kila siku, usimamizi na utunzaji wake lazima uzingatie uwiano wa matumizi yote kwa ujumla wake.
 
HALI YA HUDUMA YA MAJI MKOANI
 

Mkoa wa Dar es Salam unapata maji kutoka mito na visima kwa matumizi ya nyumbani, viwanda, bustani, mifugo, usafi na Mazingira. Eneo kubwa linalopata maji linahudumiwa na Kampuni ya DAWASCO (Dar es salaam Water Supply and Sewerage Company) ambayo imepewa mkataba na Mamlaka ya Maji Safi na Maji taka Dar es Salaam, DAWASA (Dar es Salaam Water Supply and Sewerage Authority). Maeneo yasiyo na mtandao wa DAWASA hupata maji kutoka visima vinavyoendeshwa na vyombo vya watumia maji, Taasisi na watu binafsi.

 

Kulingana na sensa ya mwaka 2012, Jiji la Dar es salaam linakadiriwa kuwa na wakazi wapatao milioni 4.3 64 ambao hupata huduma ya maji kutoka katika vyanzo vya mto Ruvu, Kizinga pamoja na maji chini ya ardhi.

 
Vyanzo vikuu vya maji kwa Mkoa wa Dar Es Salaam ni mito ya Ruvu na Kizinga pamoja na Visima, Mahitaji ya maji kwa wakazi wa Dar es Salaam na baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Pwani ni wastani wa lita million 450 kwa siku ambapo uwezo wa uzalishaji ni lita million 388 kwa siku . Maji yanayozalishwa yanakidhi mahitaji kwa asilimia 56.5 kwa wastani wa saa nane kwa siku .
 

Maeneo yasiyohudumiwa na Mtandao wa DAWASA hupata maji kutoka Miradi inayoendeshwa na Taasisi, Sekta binafsi na Jumuiya za Watumia maji kwa usimamizi wa Halmashauri na DAWASA.

 
Hali ya Upatikanaji Huduma ya Maji

Hali ya upatikanaji wa Huduma ya Maji kwa wakazi wa Dar es Salaam hivi sasa ni asilimia 72%. Maeneo yasiyohudumiwa na Mtandao wa DAWASA hupata maji kutoka Miradi inayoendeshwa na Taasisi, Sekta binafsi na Jumuiya za Watumia maji kwa usimamizi wa Halmashauri na DAWASA. Chanzo kikubwa cha maji haya ni visima. Hadi kufikia mwezi Septemba 2016 jumla kuna visima virefu 676 vya jamii vilivyopo katika Mkoa wa Dar es salaam. (Ilala 316 , Temeke 231 na Kinondoni 129). Aidha, kuna visima vya taasisi na watu binafsi visivyopungua 600 katika maeneo mbalimbali ya Mkoa. Maji yanayozalishwa na visima vya taasisi na watu binafsi yanafikia lita za ujazo million 53 kwa siku ambapo yanayokidhi mahitaji kwa asilimia 16.2 tu ya wakazi wote wa Jiji.

 

Kutokana na ufinyu wa mtandao, upatikanaji wa maji katika Jiji la Dar es Salaam hautoshelezi mahitaji, huduma ya maji hutolewa kwa mgawo. Maeneo machache (20%) yaliyopo hasa katika Wilaya ya Kinondoni hupata huduma ya maji kwa saa kati ya 16–24 wakati zaidi ya asilimia 40 hupata maji kwa mgawo wa wastani wa saa kati 3–8 kwa siku.

Takribani asilimia 40 ya eneo la Mkoa halina mtandao wa mabomba kutokana na uwekezaji mdogo, hivyo kulazimika kutumia visima kama vyanzo vikuu vya huduma ya maji. Wilaya ya Temeke ndiyo yenye kiwango cha chini (10 %) cha upatikanaji wa mtandao wa bomba kutokana na kuwa mbali na mtandao wa maji kutoka Ruvu na pia maeneo mengi ni mapya yakiwa ni makazi holela yasiyopimwa na yaliyo pembezoni. Maeneo hayo yaliendelezwa kuanzia miaka ya 1980 .

Matarajio ya Mkoa ni kutoa huduma ya majisafi na salama kwa asilimia 95 kwa wakazi wa Jiji, asilimia 30 uondoshaji wa majitaka katika Mkoa wa DSM ifikapo mwezi Desemba 2019/20.

 

 

 
 
 
 
Kisima Chenye pampu, Tanki na kituo cha kuchotea maji
 

Mpango wa Kuongeza Upatikanaji wa Huduma ya Maji

 

Mipango ya Miradi inayotekelezwa na DAWASA

 

DAWASA wanatekeleza miradi mikubwa ili kuongeza upatikanaji wa huduma ya Maji katika Mkoa wa Dar es salaam Miradi hiyo ni pamoja na:
•  Upanuzi wa Mtambo wa Ruvu Chini na ujenzi wa bomba kuu kutoka Ruvu Chini hadi matanki ya Chuo Kikuu cha Ardhi.

•  Upanuzi wa chanzo cha Ruvu Juu na ujenzi wa bomba kuu hadi matanki ya Kibamba na Kimara.

•  Mradi wa visima virefu 20 Kimbiji na Mpera na Uchimbaji wa Visima vya Majaribio.

•  Mradi wa kupunguza upotevu wa maji (Non Revenue Water -NRW)

•  Mradi wa Upanuzi wa Mfumo wa Kusambaza majisafi.

•  Mradi wa Uboreshaji Mfumo wa Uondoaji Majitaka (Upanuzi wa Miundombinu ya majitaka na ujenzi wa mfumo mpya)

•  Miradi ya visima vya dharura katika maeneo yasiyo na maji ya bomba

 

Mipango ya Miradi ya Matokeo Makubwa Sasa” BRN” inayotekelezwa na Halmashauri za Manispaa.

 

Mkoa wa Dar es salaam unatekeleza jumla ya miradi 41 ya visima vya maji katika Halmashauri za Manispaa ya Ilala, Kinondoni na Temeke chini ya mpango wa BRN katika sekta ya Maji hususani Maji Vijijini ambayo ni mojawapo ya Sekta 6 zinazotekeleza Mpango wa BRN. Miradi yote iliyokuwa inatekelezwa chini ya Programu ya Maji (RWSP) katika Mkoa wa Dar es salaam iliingizwa katika mpango wa utekelezaji wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
 
Miradi Mingine inayotekelezwa kwenye Halmashauri

 

 

Kupitia bajeti za Halmashauri (Own Souce, UNICEF, LGCGD, BTC, WATAID, na mfuko wa Jimbo) Halmashauri zote tatu zinaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maji

 
 

Hali ya Uondoshaji Majitaka Mkoa wa Dar Es Salaam

 

Mfumo wa kuondosha majitaka Jijini Dar es salaam unahudumia asilimia 10 tu ya wakazi wote wa Jiji. Mfumo wa Katikati ya Jiji unamwaga maji baharini na mifumo mingine iko Lugalo, Chuo Kikuu cha DSM, Mwenge, Kijitonyama, Mikocheni, Kurasini, Buguruni, Uwanja wa Ndege, Airwing, Barabara ya Nyerere (Tazara), Vingunguti na Ubungo. Mifumo hii inamwaga majitaka katika mabwawa yaliyoko maeneo hayo.
Maeneo yasiyo na mfumo rasmi wanatumia vyoo vya shimo na septik tanks ambapo yakijaa majitaka huchukuliwa na kupelekwa kwenye mabwawa kwa ajili ya kusafisha

 
 
 
         
 
Maji [ Nyumbani ]   Rudi juu
 
     
Copyright © 2007 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, TEL: 022 - 2203156/2203158, FAX: 022-2203213