JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA - OFISI YA WAZIRI MKUU - TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA      
 
     
 
     
MAENDELEO YA JAMII
 
Jamii [ Jinsia ] [ Watoto ] [ Nyumbani ] au
 
 
Utangulizi
 
 

Maendeleo ya jamii ni mchakato wa kujenga jamii endelevu,yenye kujiamini, kujituma na uwezo wa kushiriki,kwa misingi ya usawa na kuheshimiana, katika kubuni,kuandaa na kutekeleza mipango ya kujiletea “maendeleo” na kutumia matokeo ya kazi zao.

 

Sekta hii ya Maendeleo ya Jamii ina jukumu la kuiwezesha jamii kujiletea maendeleo. Baadhi ya malengo makuu ya sekta ni:-

 • kuiwezesha jamii kutambua uwezo ilionao na kutumia raslimali zilizopo kutatua matatizo yao .
 • kuongeza ushiriki wa makundi yote katika jamii (wanawake, wanaume, watoto, wazee, vijana n.k) katika shughuli za maendeleo ili waweza kubuni na kuanzisha miradi ambayo ni endelevu na itakayowawezesha kujipatia au kujiongezea kipato kwa miradi iliyoanzishwa na mtu mmoja mmoja, kikundi au jamii kwa ujumla wao. Aidha,
 • uhamasisha jamii kuhusu usawa wa kijinsia ili kuwezesha wanawake na wanaume kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia mahitaji ya kijinsia.
 

Shughuli Zinazotekelezwa

 

Miongoni mwa shughuli zinazotekelezwa na sekta ya Maendeleo ya Jamii katika Mkoa wa Dar es Salaam ni zifuatazo:-

 
 • Kujenga uelewa wa wananchi ili waweze kushiriki shughuli mbalimbali za kujiletea maendeleo yao kwa njia ya kujitegemea na kuwasaidia kupanga mipango inayotekelezeka.
 • Kuhamasisha wananchi kujiunga katika vikundi vya kijamii na SACCOS ili kuanzisha na kutekeleza shughuli za uzalishaji mali zenye kuchangia kuinua hali zao za maisha.
 • Kuelimisha jamii kuhusu UKIMWI, athari zake na umuhimu wa wao kushiriki katika mapambano dhidi ya janga hilo .
 • Kuelimisha jamii kuhusu kuondokana na mila potofu na imani za kishirikina zinazochangia kuzorotesha maendeleo.
 
 
 
 
Mafanikio
 
 • Wananchi wanaelimishwa katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutambua fursa au rasilimali walizo nazo katika kujiletea maendeleo yao . Hii imefanyika kupitia mfumo wa uandaaji wa mipango wa O&OD ambapo Halmashauri za Manispaa zote tatu mipango yake imeibuliwa na wananchi.
 • Mfuko wa kuwaendeleza wajasiriamali wadogo ujulikao kama “Kikwete Fund” umetoa changamoto kubwa ambapo Mkoa wa Dar es Salaam kwa mwaka 2007 ulipatiwa zaidi ya Shilingi bilioni 2.5 kwa ajili ya kukopesha wajasiriamali kupitia benki za NMB, CRDB na SACCOS mbalimbali. Hadi kuishia Desemba 2007, jumla ya wananchi 1,966 wakiwemo wanawake 805 na wanaume 1,161 walikopeshwa. Mikopo iliyotolewa hadi wakati huo ilikuwa na thamani ya shilingi Bilioni 1.9.
 • Uanzishwaji wa vikundi na Elimu kwa Wajasiriamali inatolewa kupitia sekta hii ambapo vikundi 5,730 vya kiuchumi vya wanawake na 2,455 wanaume vimeanzishwa. Shughuli ambazo vikundi hivi vinafanya ni uuzaji wa vyakula, ususi, ufumaji, uhunzi, uzalishaji wa mazao na usindikaji wa bidhaa mbalimbali
 • Usawa wa kijinsia katika elimu unazingatiwa ambapo watoto wa kike wameendelea kupata elimu sawa na wakiume. Mwaka 2008, wasichana 33,801 na wavulana 32,008 walimaliza elimu ya msingi na kati yao wasichana 17,823 na wavulana 22,536, walifaulu. Waliojiunga na elimu ya Sekondari ni wasichana 10,280 na wavulana 10,280
 • Ushiriki wa sekta ya Maendeleo ya Jamii umewezesha jamii kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo hususan ujenzi wa shule za Sekondari za Kata zinazofikia 100 kutoka 6 mwaka 2005
     
     
 
         
 
Jamii [ Jinsia ] [ Watoto ] [ Nyumbani ] au
Rudi juu
 
     
Copyright © 2007 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, TEL: 022 - 2203156/2203158, FAX: 022-2203158