`
  JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA - OFISI YA WAZIRI MKUU - TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA      
 
     
 
 
HALMASHAURI YA MANISPAA YA TEMEKE
 
[ Nyumbani ]
 
 
[ MKUU WA WILAYA ] [ WABUNGE ] HALMASHAURI YA MANISPAA YA TEMEKE [ KATA & MITAA ]
                           
 
 
Utangulizi
 

Halmashauri ya Manispaa ya Temeke ilianzishwa rasmi tarehe 1/2/2000 . Ni moja kati ya Halmashauri sita zinazounda Jiji la Dar es Salaam. Ipo upande wa kusini wa Mkoa wa Dar es Salaam ambapo kwa upande wa mashariki inapakana na Bahari ya Hindi, kusini inapakana na Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani na upande wa kaskazini na magharibi inapakana na Manispaa ya Ilala.

Idadi ya Watu

Kwa mujibu wa Sensa ya Taifa ya mwaka 2012 Manispaa ya Temeke ina jumla ya wakazi 1,368,881. Kati ya hao wanaume ni 669,056 na wanawake ni 699,825.

 
 
Utawala
 

Halmashauri ya Manispaa Temeke imegawanyika katika Tarafa 2 ,ambazo ni Mbagala na Chang'ombe. Aidha zipo Kata 23 na jumla ya Mitaa 142.

 
Shughuli za Kiuchumi na Kijamii
 

Kimgawanyo Temeke, ikiwa ni sehemu ya Jiji la Dar es Salaam inamiliki eneo kubwa la Viwanda na biashara hapa Nchini. Inavyo jumla ya Viwanda 198 ambapo viwanda 40 ni vikubwa na 158 ni Viwanda vya kati ambavyo ndivyo chanzo kikubwa cha ajira ya wakazi wake pamoja na wale wa Halmashauri nyingine za Ilala na Kinondoni.
Kufuatia Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2002 takwimu zinaonyesha kwamba asilimia 49 ya wakazi wameajiriwa na kujiajiri kwenye Sekta Rasmi na Isiyorasmi ikifuatiwa na asilimia 20 ya wakazi ambao wameajiriwa katika kazi za Ofisini.
Aidha asilimia 13 ya wakazi wote hujishughulisha na Kilimo cha Mazao ya Chakula, Biashara na Mbogamboga

 

ELIMU

Halmashauri ya Manispaa ya Temeke ina jukumu la kutoa elimu kuanzia shule za awali, Msingi na Sekondari. Kuna vyuo mbalimbali vilivyoko chini ya Wizara, Taasisi au watu binafsi vinavyotoa mafunzo ya taaluma mbalimbali kama vile VETA.

Elimu ya Awali

Halmashauri ya Manispaa ya Temeke ina shule/vituo vya awali 100 kati ya hivyo 85 ni vya serikali na 15 visivyo vya serikali.

 
Elimu ya Msingi
 

Manispaa ya Temeke ina jumla ya shule za msingi 114; Shule 100 ni za serikali na 14 zisizo za serikali

 
Elimu ya Sekondari
 
Katika Manispaa ya Temeke zipo jumla ya shule za Sekondari 64 ambazo kati ya hizo, shule 34 ni za Serikali na shule 31 zisizo za serikali.
 

Kilimo na Mifugo

 

Sekta ya kilimo na mifugo imeendelea kuwa ndiyo msingi katika kukuza mapato ya familia na jamii kwa ujumla. Sekta iliweka mkazo katika mafunzo kwa wakulima na wafugaji kwa lengo la kuwaongezea utaalamu ili waweze kutumia mbinu za kisasa za kilimo na ufugaji bora.
Aidha Mafunzo hutolewa kwa wakulima wa mazao mbalimbali na wafugaji, Mafunzo hayo yanahusu maeneo yafuatayo: Kilimo:

  • Utunzaji wa mashamba ya Korosho
  • Ubanguaji wa Korosho.
  • Kilimo cha mbogamboga na matumizi ya mbolea ya viwandani na madawa ya kuuwa wadudu.
  • Ugonjwa wa kunyong'onyea kwa Minazi na athari zake.
  • Umwagiliaji kwa kutumia pampu ya zege (Concreate Pedal Pump)
  • Uanzishaji na uimarishaji wa vikundi vya wakulima.

Mifugo:

  • Uboreshaji wa kuku wa kienyeji kwa kutumia majogoo bora aina ya Rhode Ireland Red (RIR).
  • Ugonjwa wa kideri ( Newcastle disease) na ndui ya kuku (Fowl Pox) athari zake na kinga.
  • Ufugaji bora wa ng'ombe wa maziwa.
  • Ufugaji bora wa mbuzi wa maziwa.
 
 
 
 
Ofisi ya Halmashauri ya Manispaa ya Temeke
 
Afya
 

Idara ya Afya katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke inatoa huduma za tiba na kinga, mbazo zinaendelea kuboreshwa katika Hospitali za binafsi na za Serikali, Aidha zipo Zahanati na Vituo vya Afya vya Serikali na watu binafsi na mashirika na taasisi mbalimbali.

Afya Kinga:
Kitengo cha Afya Kinga kinatoa huduma mbali mbali ikiwa ni pamoja na usimamizi wa Afya na Mazingira, udhibiti wa magonjwa ya kuambukiza na milipuko.

 
Maji

Wakazi wa Manispaa ya Temeke wanapata huduma ya maji kutoka katika vyanzo vya Maji ya mtandao wa mabomba ya DAWASA, na katika Visima vifupi vya kati na visima virefu; maji mengine kutoka katika chanzo cha mto Kizinga -Mtoni (DAWASCO)

Mahitaji halisi ya maji ni kiasi cha lita za ujazo 73. 827 Milioni kwa siku, wakati kiasi halisi kinachopatikana ni lita za ujazo 55.27 milioni kwa siku sawa na 75% tu ya mahitaji ya wakazi wa Manispaa ya Temeke wanaopata huduma ya maji safi na salama karibu na makazi yao kwa umbali uziozidi mita 400.

Kiasi hiki kimeongezeka kutoka lita za ujazo 34.945 Milioni kwa siku hadi kufikia lita za ujazo 55.276 Milioni kwa siku. Ongezeko hilo ni sawa na asilimia 63%. Ongezeko hili limetokana na juhudi za Halmashauri kwa kushirikiana na wafadhili pamoja na wananchi kwa kuongeza Idadi ya visima.

Katika kukabiliana na upungufu wa Maji na kuhakikisha kuwa wananchi wanapata maji safi na salama ili kuepukana na magonjwa yanayosababishwa na ukosefu wa maji safi na salama kama kuharisha na kipindupindu, Halmashauri kwa kushirikiana na shirika la WATER AID, miradi ya maji 15 imetekelezwa na inaendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali katika Halmashauri.

 
 
 
 

Hifadhi ya Mazingira

Manispaa ya Temeke imebahatika kuwa na utajiri mkubwa wa maliasili na utalii. Temeke imezungukwa na ufukwe wa bahari wenye urefu wa km. 70. ukanda huu ni kivutio kikubwa cha utalii. Aidha, Manispaa ina machimbo ya Mchanga, Kifusi, Kokoto, Mawe na Chokaa .

Maeneo yanayotoa madini hayo na aina yake ni kama ifuatavyo:
•  Chamazi Mchanga.
•  Mbande Mchanga.
•  Kimbiji Mchanga.
•  Toangoma - Mchanga
•  Mjimwema Kokoto, Mawe, na Kifusi.

Kutokana na ukuaji wa kasi wa shughulli za ujenzi katika Manispaa ya Temeke na maeneo mengi ya Jiji la Dar Es salaam , mahitaji ya rasilimali hii yanaongezeka mwaka hadi mwaka hasa ukizingatia kwamba Manispaa ina rasilimali nyingi zenye ubora wa hali ya juu kulinganisha na Manispaa nyingine za Jiji la Dar Es salaam. Ili kuepuka wananchi kuchimba madini hayo kiholela katika maeneo yasiyostahili na kuleta madhara makubwa Kimazingira na Kiuchumi, imependekezwa kuwe na maeneo maalumu ya uchimbaji madini hayo ili kudhibiti uharibifu wa mazingira na upotevu wa mapato.

Baadhi ya maeneo yaliyofungwa ili kudhibiti uharibifu wa mazingira na upotevu wa mapato ni Kisarawe II, na Vijibweni kwa Manispaa ya Temeke.

Pia kufungwa kwa machimbo ya Kunduchi, Manispaa ya Kinondoni ambayo yalikuwa yanatoa madini ya kokoto na kifusi kwa kiasi kikubwa kwa jiji la Dar es Salaam, imepelekea kutafutwa eneo jipya la Madini ambalo imependekezwa machimbo hayo yahamie Mbutu na Mwongozo katika Manispaa ya Temeke. Tafiti zimefanyika kwamba maeneo hayo yatakidhi mahitaji ya kokoto na kifusi kwa jiji la Dar Es Salaam na uharibifu wa mazingira na upotevu wa mapato utakuwa rahisi kudhibitiwa.

 

Tembelea Tovuti ya Halmashauri ya Manispaa ya Temeke
 
 
     
[ Nyumbani ]   Rudi juu
 
     
Copyright © 2007 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, TEL: 022 - 2203156/2203158, FAX: 022-2203158