JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA - OFISI YA WAZIRI MKUU - TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA      
 
     
 
 
HALMASHAURI YA MANISPAA YA KINONDONI
 
[ Nyumbani ]
 
 
[ MKUU WA WILAYA ] [ WABUNGE ] HALMASHAURI YA MANISPAA YA KINONDONI[ KATA & MITAA ]
                           
Utangulizi
 

Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni ina ukubwa wa kilomita za mraba 320. Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imepakana na Wilaya ya Bagamoyo upande wa Kaskazini, upande wa Kaskazini Mashariki inapakana na Bahari ya Hindi, upande wa Kusini inapakana na Manispaa ya Ilala, upande wa Kusini Magharibi inapakana na Wilaya ya Kisarawe na upande wa Magharibi inapakana na Wilaya ya Ubungo.

 
Idadi ya watu
Kutokana na matokeo ya sensa ya mwaka 2012 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni ina idadi ya watu 1,775,049. kati ya hao Wanaume 860,802 na wanawake 914,247. ikiwa ongezeko la watu kwa wastani wa aslimia tano.
 
Utawala

Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imegawanyika katika Tarafa 2, Kata 20, Jumla ya Mitaa ni 112, Idadi ya Majimbo ya Uchaguzi ni mawili (2) ambayo ni Kawe na Kinondoni Mstahiki Meya ni Kiongozi Mkuu na Mkurugenzi wa Manispaa ni Mtendaji Mkuu kwa upande wa Serikali za Mitaa. Manispaa inaongozwa na Baraza la madiwani.

 
 
Hali ya Uchumi:

Uchumi wa wakazi wa Manispaa unategemea biashara kubwa na ndogo, ufugaji mdogo mdogo, kilimo cha bustani, viwanda vidogo, viwanda vikubwa na utalii.

Inakadiriwa kuwa asilimia 95 ya wakazi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni wamejiajiri katika sekta isiyo rasmi na asilimia 5 ya wakazi wameajiriwa katika Taasisi mbalimbali za Umma.

 

Elimu ya Msingi

Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni ina jumla ya madarasa ya awali 232 zikiwa 127 katika shule za Serikali na 105 zisizo za Serikali. Idadi ya shule za Msingi ni 228 zikiwemo 138 za Serikali na 90 za Binafsi. Aidha kuna jumla ya shule za Sekondari 145 zikiwemo 46 za Serikali na 96 zisizo za Serikali. Vipo vituo 80 vya Elimu ya Watu Wazima ambavyo vinajumuisha madarasa ya MEMKWA 60, na madarasa ya MUKEJA 40.

 

Hali ya uandikishaji katika Shule za Msingi:

Kumekuwa na ongezeko katika uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la kwanza tangu Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) ulipoanza nchini mwaka 2002. Hii imetokana na kuhamasika kwa jamii katika suala zima la kuandikisha watoto kuanza shule, pia kuongezeka kwa vyumba vya madarasa, nyumba za walimu na upatikanaji wa miundombinu mingine ya vyoo, madawati, walimu na vifaa vya kufundishia na kujifunzia.

 

Huduma ya Afya
 

Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imeendelea kutoa huduma za Afya kwa kutumia Hospitali yake ya Mwananyama, Vituo vya Afya na Zahanati zake Huduma ya Afya katika vituo vya tiba hutolewa kwa nia ya kuboresha tiba na kinga za magonjwa mbalimbali ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza. Hospitali ya wilaya huudumia wagonjwa kati ya 900 na 1,100 kwa siku.

AFYA KINGA:
Kitengo cha Afya Kinga kinatoa huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na usimamizi wa Afya na Mazingira, udhibiti wa magonjwa ya kuambukiza na milipuko. Pia kitengo hiki huhamasisha na kutoa elimu ya afya kwa jamii kwa kutumia vipaza sauti, video, vipeperushi, ngonjera, nyimbo na maigizo

 
 

KILIMO NA MIFUGO

•  Manispaa ya Kinondoni ina eneo la kilomita za mraba 531 sawa na Hekta 531,000
•  Eneo linafaa kwa kilimo ni Hekta 39,980 eneo lililolimwa na kupandwa ni Hekta 4022

 
 

 

 

Ofisi ya Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni

 
 
Maliasili na Uvuvi
 
Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni inaendelea kutunza na kuhifadhi mazingira kwa kuotesha na kupanda miti ya vivuli, mbao na matunda kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali. Miche mbalimbali imeoteshwa na kupandwa kwenye maeneo ya Kata, Mitaa na Taasisi za Umma zikiwemo Kambi za Jeshi, maeneo ya akiba za barabara, Shule za Msingi na Sekondari.
 
Vipo vikundi vya wajasiriamali 238 vya utunzaji wa bustani na vitalu vya miche. Aidha, shughuli za uvuvi ziliendelea kufanyika katika mwambao wa bahari ya Hindi. Manispaa ina jumla ya wavuvi 1,701 na vyombo vya uvuvi 370 . vipo vituo vya kupokelea samaki 4 ambavyo ni Msasani, Kunduchi, Ununio na Mbweni. Vipo vikundi 3 vya uvuvi vilivyosajiliwa vyenye jumla ya wanachama 600 . yapo mabwawa ya kufugia samaki yapatayo 16 yanayomilikiwa na wananchi. Vipo vikundi 8 vya ufugaji nyuki na watu binafsi wenye jumla ya mizinga 516 (mizinga ya kisasa 469 na 67 ya kiasili)


Aidha mradi wa Uwiano na Usimamizi wa Mazingira ya Pwani (KICAMP) unasimamia na kutunza rasilimali za fukwe na bahari katika kata za Kunduchi, Mbweni na Bunju.

Ushirika na Masoko
Kitengo cha Ushirika katika Halmashauri ya Manispaa kina idadi ya vyama vya Ushirika 156. Kati ya hivyo, vyama 130 ni vya Akiba na mikopo. Vyama hivi vinatoa huduma za kibenki kwa wanachama wake ambazo ni kuweka akiba na kisha kukopa, hivyo kuwawezesha kuendesha shughuli mbali mbali za kiuchumi yaani biashara na maendeleo. Jumla ya vyama 26 vilivyobaki ni vyama vinavyotoa huduma mbali mbali kwa wanachama wake kwa mfano ushirika wa nyumba n.k.
Halmashauri imeendelea kutoa elimu kwa vyama vya ushirika ili viwe imara na endelevu kwa vyama 25.
 
 
Huduma ya Maji:

 

Mahitaji ya maji katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kwa sasa ni mita za ujazo 170,760 kwa siku lakini huduma inayopatikana kutoka katika mifumo ya maji ya DAWASA ni chini ya asilimia 45 ya mahitaji halisi. Kiasi hicho cha huduma ya maji kinapatikana katika maeneo yenye miundombinu ya mabomba ya DAWASA tu. Kutokana na hali hiyo, Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imekuwa inajenga miradi ya maji ambapo kwa sehemu kubwa inategemea visima virefu kama vyanzo vya maji mbadala katika maeneo yasiyo na mifumo ya maji ya DAWASA.

 
 
 

 
 

.

   
[ Nyumbani ]   Rudi juu
 
     
Copyright © 2007 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, TEL: 022 - 2203156/2203158, FAX: 022-2203213